In Summary

• Hamo alisema kwamba anawaombea wafuasi wake kuwa na rafiki kama naibu wa rais William Ruto wa kuwazaba makofi wakitaka kukata tamaa ya maisha.

Hamo The Professor Mchekeshaji wa Churcvhill Show
Image: Facebook

Mchekeshaji wa Churchill Show ambaye pia anajiongeza kama mwanamuziki kwa jina Hamo The Professor amewachekesha wengi kwenye mitandao ya kijamii baada ya kuzua utani kuhusu suala linalozidi kutokota nchini kutokana na sauti ya naibu rais William Ruto iliyovujishwa kwamba alitaka kumzaba kofi rais Uhuru Kenyatta mwaka 2017.

Akiandika kwenye ukurasa wake wa Facebook, Hamo alisema kwamba anaombea mashabiki na wafuasi wake wote kuwa na Rafiki kama Ruto ambaye atakupiga kofi wakati unaelekea kukata tamaa katika juhudi zako.

“Ombi langu ni kwamba upate Rafiki kama William Samoei Ruto ambaye atakuzaba kofi moja la moto wakati unaelekea kukata tamaa ya kufukuzia ndoto zako,” aliandika Hamo The Professor.

Watu wengi walionekana kutoelewa ucheshi na utani katika maneno haya ambapo waligeuza ukurasa wa Hamo kama jukwaa la kisiasa la kutanuliana vifua huku baadhi wakimtetea naibu rais William Ruto kwa kitendo hicho alichotaka kukifanya kwa rais huku wengine wakimkosoa vikali.

“Angemuacha tu Uhuru akate tamaa ya kuwa rais kwa mkondo wa pili, ametuharibia uchumi sana hiyo miaka mitano ya mwisho. Ruto ni sharti aombe Wakenya msamaha kwa kumlazimisha Uhuru kuwania kipindi cha pili,” aliandika mmoja kwa jina Gadys Wambui.

Professor Hamo, ambaye jina lake halisi ni Herman Gakobo Kago ni mmoja kati ya wachekeshaji wenye weledi na uelewa mkubwa wa Sanaa ya ucheshi nchini ni mmoja kati ya wachache ambao wana uwezo mkubwa wa kutumia matukio yanayozungumziwa sana katika muktadha wa ucheshi na kufanikiwa kuwavunja mbavu mashabiki wake.

Sauti ya Ruto akisema alimlazimisha rais Kenyatta kuwania katika uchaguzi wa marudio wa 2017 baada ya majaji wa mahakama ya juu kuharamisha uchaguzi wa kwanza ilivujishwa na mbunge wa Suna Mashariki Junet Mohammed katika hafla moja ya kisiasa kwenye kaunti ya Homa Bay wiki iliyopita.

Katika mkanda huo wa sauti, Ruto anasikika akisema kwamba baada ya rais Uhuru Kenyatta kuwa na msimamo kwamba hatoshiriki tena uchaguzi wa marudio, alikasirika na nusra amzabe kofi ila baadae walimbembeleza kwa ushirikiano wa viongozi kadhaa na rais akakubali kuwania.

View Comments