In Summary

• Mahakama ya Juu ilitoa kile kilichoonekana kama onyo kwa maafisa wa serikali ikisema kwamba wanapaswa kuheshimu sheria, haswa sura ya sita ya katiba.

• Awali Sonko alikuwa amewasilisha rufaa hiyo katika mahakama kuu baada ya Mahakama ya Rufaa na Mahakama Kuu kuidhinisha kuondolewa kwake afisini na Seneti.

• Mnamo Desemba 3, 2020, sonko aling’atuliwa mamlakani na wakilishi wadi 88 wa bunge la kaunti ya Nairobi.

Aliyekuwa gavana wa Nairobi, Mike Sonko
Image: Facebook

Aliyekuwa Gavana wa Nairobi Mike Mbuvi Sonko hataruhusiwa kuwania kiti chochote cha uchaguzi au kuteuliwa katika afisi ya serikali nchini Kenya, uamuzi mpya wa Mahakama ya Juu unamaanisha hivyo.

Kufuatia uamuzi wa mahakama ya Juu, Sonko atafeli moja kwa moja mtihani wa uadilifu ili kuhitimu kibali cha kuwania kiti cha uchaguzi katika uchaguzi wowote nchini Kenya au kuteuliwa.

Hii ni kwa kuzingatia katiba ya Kenya, Sura ya Sita Ibara ya 75 (3), inayosema; Mtu ambaye ameachishwa kazi au kuondolewa madarakani kwa kukiuka masharti yaliyoainishwa katika ibara ya (2) hatastahili kushika wadhifa wowote wa Serikali.

Wakati ikithibitisha uamuzi wake, Mahakama ya Juu ilitoa kile kilichoonekana kama onyo kwa maafisa wa serikali ikisema kwamba wanapaswa kuheshimu sheria, haswa sura ya sita ya katiba.

“Sura ya Sita ya Katiba haikutungwa bure au kwa sababu za urembo, mamlaka aliyopewa ofisa wa Serikali ni dhamana ya umma inayopaswa kutekelezwa kwa njia inayoonyesha heshima kwa wananchi; inaleta heshima kwa taifa na heshima kwa ofisi, na kukuza imani ya umma katika uadilifu wa afisi hiyo. Inampa afisa wa Serikali jukumu la kuwatumikia wananchi, badala ya mamlaka ya kuwatawala.

Awali Sonko alikuwa amewasilisha rufaa hiyo katika mahakama kuu baada ya Mahakama ya Rufaa na Mahakama Kuu kuidhinisha kuondolewa kwake afisini na Seneti.

Uamuzi wa Mahakama ya Juu sasa unabatilisha uamuzi wa Mahakama Kuu ya Mombasa ambayo ilikuwa imeagiza IEBC kumwidhinisha Sonko kuwania ugavana wa Mombasa.

Mnamo Desemba 3, 2020, sonko aling’atuliwa mamlakani na wakilishi wadi 88 wa bunge la kaunti ya Nairobi.

Uamuzi huo kisha ulipelekwa kwa Seneti mnamo Desemba 17, 2020, ambapo seneti iliidhinisha azimio la kumwondoa afisini.

Mapema mwaka huu, Sonko alienda katika Mahakama ya Juu kupinga kuondolewa kwake.

Hii ilikuwa baada ya Mahakama ya Rufaa kukubaliana na uamuzi wa Mahakama Kuu kwamba aliondolewa kisheria mwaka 2020.

Mahakama pia iligundua kuwa Seneti ilimsikiliza Sonko kabla ya kuafikia kwamba alifaa kuondoka ofisini.

Kujiunga na siasa 

Sonko aliingia katika siasa mnamo Septemba 2010, alipojiunga na kinyang'anyiro cha kiti cha ubunge cha Makadara wakati wa uchaguzi mdogo.

Alishinda kwa tiketi ya chama cha Narc Kenya kinachoongozwa na Martha Karua.

Ni maisha yake ya kifahari bungeni yaliyomfanya kuwa maarufu nchini Kenya na kipenzi cha vijana.

Kukaa kwake Narc Kenya, hata hivyo, hakudumu baada ya kufukuzwa mnamo Agosti 2011.

Hii ni baada ya kudaiwa kumfanyia kampeni mgombeaji wa PNU - ambaye sasa ni mbunge - Yusuf Hassan, badala ya kumpigia kampeni mgombeaji wa chama chake, Brian Weke, katika uchaguzi mdogo wa Kamukunji.

Alijiunga na chama cha TNA kabla ya uchaguzi wa 2013 na kushinda kiti cha Seneta wa Nairobi.

Baada ya miaka mitano akiwa seneta alijitosa katika kinyangányiro cha Ugavana mwaka 2017 kwa tikiti ya chama cha Jubilee na kushinda.

Hata hivyo, muda wake wa kukaa katika Jumba la City Hall ulikatizwa kufuatia kuondolewa kwa kura ya kutokuwa na imani.

Sonko amekuwa  akilenga kurejea uongozini na anatafuta kumrithi Gavana wa Mombasa Ali Hassan Joho.

View Comments