logo

NOW ON AIR

Listen in Live

Mike Sonko amhimiza Kalonzo kumtema Raila na kumfuata Kenya Kwanza

Sonko alimshutumu Raila kwa kuwanyima viongozi wa jamii ya Kamba nyadhifa katika serikali yake.

image
na Radio Jambo

Makala31 July 2022 - 05:31

Muhtasari


•Sonko aliwabainishia Wakamba kuwa hakuna ugomvi wowote kati yake  na Kalonzo licha ya kukigura chama chake.

•Sonko alisema kuna mazuri mengi kwa Wakamba katika Kenya Kwanza tofauti na kwa wapinzani wao Azimio.

Aliyekuwa gavana wa Nairobi, Mike Sonko ametoa wito kwa kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka kumfuata kwenye muungano wa Kenya Kwanza.

Jumamosi Sonko aligura chama cha Wiper na kujiunga na UDA yake William Ruto.

Ruto ambaye anapeperusha bendera ya muungano huo katika kinyang'anyiro cha urais ndiye aliyempokea Sonko.

"Tunamkaribisha Mike Sonko kwa Kenya Kwanza, timu inayoshinda," Ruto aliandika kwenye ukurasa wake wa Facebook.

Naibu rais aliambatanisha ujumbe wake na picha zilizoonyesha akimpokea Sonko katika ofisi zake jijini Nairobi.

Baadae siku hiyo Sonko aliandamana na timu ya Kenya Kwanza kupeleka kampeni zao katika maeneo ya Ukambani.

Akizungumza mjini Machakos, Sonko aliwabainishia wakazi kuwa hakuna ugomvi wowote kati yake  na Kalonzo licha ya kukigura chama chake.

"Mimi sina shida na ndugu yetu Stephen Kalonzo Musyoka. Huyu ndugu yangu Ruto hana shida na Stephen Kalonzo Musyoka," Sonko alisema.

Gavana huyo wa zamani alitumia fursa hiyo kumwalika Kalonzo kwenye muungano huo wa Kenya Kwanza.

Kalonzo anafahamika kuwa mmoja wa viongozi wakuu katika eneo la Ukambani na kwa sasa yupo upande wa Azimio-One Kenya.

"Vile mmeniombea Mungu nikarudi kwa hustler, naomba muombe Mungu afungue macho na masikio ya ndugu yetu Stephen Kalonzo Musyoka akuje hii pande tumalize mchezo huu," Alisema.

Sonko alisema kuna mazuri mengi kwa Wakamba katika Kenya Kwanza tofauti na wapinzani wao wa Azimio ambapo Kalonzo ameahidiwa wadhifa wa Waziri Mkuu.

Alimshutumu mgombea urais wa Azimio Raila Odinga kwa kuwanyima viongozi wa jamii ya Kamba nyadhifa katika serikali yake.

"Huyu babu alipotaja serikali yake pale KICC alimpatia Joho kama waziri wa Ardhi.  Nyinyi mnajua Ngilu amepatiwa nini? Ngilu amezama. Mnajua Kivutha Kibwana amepatiwa nini? Hakuna.," Alisema.

Gavana huyo wa zamani aliwahakikishia wakazi nafasi kadhaa kati ya alizoahidiwa katika serikali ya Ruto.

Akitangaza kuhamia kwake kwenye Kenya Kwanza siku ya Jumamosi, Sonko alifichua kuwa alitia saini makubaliano na Kenya Kwanza kuhusu nyadhifa kadhaa serikaini ikiwa muungano huo utatwaa ushindi.

"Zifuatazo ni nafasi zinazotolewa kwangu pamoja na watu wangu kama zilivyonaswa katika makubaliano ya uchumba/MOU; Waziri mmoja katika serikali ya Kitaifa, Makatibu watatu wa wizara katika serikali ya Kitaifa , Mabalozi Wanne, CEC watatu katika kaunti ya Mombasa, Maafisa Wakuu watatu katika Kaunti ya Mombasa, CEC wawili katika kaunti ya Nairobi, Maafisa Wakuu watatu Kaunti ya Nairobi," Alisema.

Pia alidokeza kuwa masaibu mengi yaliyokumba azma yake ya kuwania ugavana Mombasa ndiyo yaliyomsukuma kuuonyesha mgongo  muungano wa Azimio-One Kenya.


RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved