In Summary

•DP Ruto alisema kwamba timu yake inashukuru kwa kuwa wameuona mkono wa Mungu katika safari yote.

•Naibu rais pia alitoa wito wa kufanyika uchaguzi wa amani, akiwataka Wakenya kuombea amani.

Huku zikiwa zimesalia siku sita kabla ya uchaguzi Mkuu, Naibu Rais William Ruto amemshukuru Mungu kwa safari ya urais aliyoianza.

Akizungumza wakati wa mkutano wa maombi katika makazi yake ya Karen, DP alisema kwamba timu yake inashukuru kwa kuwa wameuona mkono wa Mungu katika safari yote. Alisema walivumilia na kushinda changamoto nyingi wakiwa njiani.

Naibu rais alidai kuwa Kenya ilikuwa inakabiliwa na vita vya kiroho ambavyo vinaweza tu kushindwa kupitia maombi ya wale wanaoamini.

"Kama timu, tunashukuru sana na tumeona mkono wa Mungu katika safari hii,"

“Katika safari yetu, tumefahamu kwamba marafiki wanaweza kukuangusha lakini Mungu hawezi. Tumefikia utambuzi wa kumwamini Mungu kwa sababu wanadamu wanaweza kukuangusha,” Ruto alisema.

Mkutano huo wa maombi ambao ulikuwa umeitishwa na mkewe, Mama Rachel Ruto uliwaleta pamoja makasisi na washiriki wakuu wa kanisa kuombea nchi kabla ya uchaguzi wa Agosti 9.

Huku akiwashukuru makasisi na waumini kwa kuhudhuria kikao cha maombi, Naibu Rais Ruto alifichua jinsi nusra akose kikao hicho kutokana na shughuli zake nyingi.

"Nilipuuza mkutano huu lakini imekuwa kile ambacho sikufikiria. Asante kwa kuja kuomba pamoja nami na timu yangu na kushiriki wakati huu wenye baraka pamoja,” alisema.

Aliendelea zaidi na kunukuu Biblia huku akiwashukuru makasisi kwa kujumuika kuombea timu yake.

"Tuna ratiba nyingi lakini Biblia inatukumbusha kwamba utafuteni kwanza ufalme wa Mungu na kila kitu kingine kitakuwa tayari," DP aliongeza.

Aidha, mgombea urais huyo wa Kenya Kwanza alitoa wito wa kufanyika uchaguzi wa amani, akiwataka Wakenya kuombea amani.

"Tunataka kila Mkenya aombe amani kwa sababu tunataka kupiga kura zetu kwa amani na hatimaye mapenzi ya Mungu yatashinda," Ruto alisema.

"Tunataka kuwaomba muendelee kutuombea na kwa ajili ya amani ya nchi... Kuna watu ambao wangetaka kuvuruga amani ya nchi yetu," aliongeza.

DP pia alitoa changamoto kwa makasisi kushirikisha kundi lao na kuwahimiza waepuke vurugu na kujitokeza kwa wingi na kutekeleza haki yao ya kidemokrasia katika kupiga kura.

Utafsiri: Samuel Maina

View Comments