In Summary

•Inadaiwa wanne hao walikuwa wakipanga kujaza karatasi za  kura kwenye masanduku ili kuwapendelea wagombeaji fulani

•IEBC imesema nafasi nne zilizoachwa wazi zitajazwa Jumatatu kabla ya uchaguzi mkuu wa Jumanne.

Mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) WAFULA CHEBUKATI
Image: EZEKIEL AMING'A

Tume ya uchaguzi na mipaka nchini imewapiga kalamu maafisa wake wanne ambao walifumaniwa katika mkutano na wagombea wawili katika kaunti ya Homa Bay.

IEBC imesema nafasi nne zilizoachwa wazi zitajazwa kabla ya uchaguzi mkuu kung'oa nanga siku ya Jumanne.

Wanne hao ambao ni pamoja na msimamizi wa kituo cha kupigia kura katika wadi ya Kanyadoto, naibu wasimamizi wawili wa vituo vya kupigia kura katika wadi hiyo na karani wa kituo cha kupigia kura katika wadi jirani ya Kwabwai, walifutwa kazi baada ya kupatikana kwenye mkutano huo haramu.

Walikuwa wakikutana katika nyumba ya mgombea mmoja wa kiti cha MCA huko Riat katika wadi ya Kanyikela. Inadaiwa walikuwa wakipanga kujaza karatasi za  kura kwenye masanduku ya kupigia kura ili kuwapendelea wagombeaji fulani wa chama cha kisiasa.

Mnamo Jumatatu, IEBC kupitia kwa afisa anayesimamia uchaguzi wa IEBC wa Homa Bay Fredrick Apopa iliwafuta maafisa hao kutokana na kosa hilo.

Apopa alisema wasimamizi hao walifutwa  kwa sababu walishiriki katika mkutano usio halali.

"Tunaajiri watu wengine kuchukua nafasi z zilizoundwa na watu walioachishwa kazi. Hawawezi kuaminiwa tena,” Apopa alisema.

Afisa huyo wa IEBC alisema watu waliotimuliwa wanaripotiwa kukutana na wanasiasa kama MCA na mwaniaji ubunge kutoka chama cha kisiasa katika eneo bunge la Ndhiwa.

Alisema bado hawajui wanne hao walikuwa wakijadili nini katika mikutano yao.

Kesi hiyo ilijulikana kwa umma baada ya wakaazi fulani kuvamia nyumba hiyo, na kuwafurusha washukiwa kabla ya kuwaita polisi kuwakamata.

Baadaye walipelekwa katika  kituo cha polisi cha Ndhiwa kwa mahojiano.

"Tunashirikiana na polisi kuwachunguza. Hatua zinazofaa zitachukuliwa dhidi yao kwa kujaribu kujihusisha na makosa ya uchaguzi,” Apopa alisema.

Baadhi ya watu watakaohojiwa ni wananchi waliowapeleka viongozi hao kituo cha polisi Ndhiwa. Matokeo ya uchunguzi yataamua iwapo watashtakiwa.

Maafisa wengine wa tume hiyo waliokuwa kwenye mkutano huo walifanikiwa kutoroka baada ya kuona umati wa watu ukiongezeka kuelekea nyumbani

View Comments