In Summary

•Awiti ambaye anawania kiti cha ugavana Mombasa kwa mara ya pili, alilaumu ulegevu wa IEBC kwa makosa ya karatasi za kupigia kura. 

•Awiti aliitaka IEBC na mashirika ya usalama kuwachukulia hatua watu ambao, alidai, walijaribu kuvuruga uchaguzi.

Gavana wa Mombasa wa VDP Hezron Awiti akipiga kura katika shule ya msingi ya Ziwa La Ng'ombe siku ya Jumanne, Agosti 9.
Image: LABAN WALLOGA

Aliyekuwa mbunge wa Nyali Hezron Awiti ametishia kuishtaki tume huru ya uchaguzi na mipaka kwa kuahirisha uchaguzi wa ugavana Mombasa.

Awiti ambaye anawania kiti cha ugavana Mombasa kwa mara ya pili, alilaumu ulegevu wa IEBC kwa makosa ya karatasi za kupigia kura. Alisema tume ya uchaguzi lilikuwa limewahakikishia Wakenya kuwa wako tayari kuendesha uchaguzi.

“Ninashauriana na wanasheria wangu kuhusu hatua inayofuata. Tumetumia pesa kufanya kampeni na watu wetu walikuwa tayari kupiga kura,” Awiti alisema.

“Ikiwa IEBC imehusika kwa hili, basi wanapaswa kuwajibika. Ikiwa ni msambazaji, wanapaswa kuwajibika."

Wajumbe wa IEBC, vyama vya kisiasa na wengine walienda Ugiriki kushuhudia uchapishaji na upakiaji wa kura za urais na nyinginezo, ingawa hawakuweza kuangalia kila kitu.

Awiti alisema alikuwa katika kituo cha kujumlishia kura eneo bunge la Mvita siku ya Jumatatu ili kuthibitisha ripoti hizo alipopata habari kuwa karatasi za kupigia kura za ugavana wa Mombasa hazikuwepo.

Jumatatu jioni, mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati alitangaza uchaguzi wa ugavana katika kaunti za Mombasa na Kakamega umesimamishwa kwa sababu ya hitilafu kwenye karatasi za kupigia kura.

Chebukati alisema kuwa tarehe mpya za uchaguzi zitatangazwa kupitia notisi ya gazeti la serikali.

Tume hiyo pia ilisimamisha uchaguzi wa wabunge katika maeneo bunge ya Pokot Kusini na Kachelia.

Awiti aliitaka IEBC na mashirika ya usalama kuwachukulia hatua watu ambao, alidai, walijaribu kuvuruga uchaguzi.

Haya yanajiri kufuatia kukamatwa kwa mgombea wa UDA eneo bunge la Mvita Omar Shallo na mwaniaji wadi ya Tudor Samir Bhalo kwa madai ya dosari.

"Inasikitisha mambo haya yanaweza kutokea wakati huu. Ninafahamu baadhi ya sehemu za Mvita zilikuwa bado hazijaanza kupiga kura kuanzia saa tisa asubuhi. Ninakwenda huko kufuatilia hali ilivyo,” alisema.

"Hizi ni dalili za wazi baadhi ya watu walikuwa wakipanga kuiba, tuna bahati uchaguzi wa ugavana umeahirishwa," alisema.

Aidha alidai kuwa baadhi ya maafisa wa IEBC walikuwa wakishirikiana na baadhi ya wawaniaji kuvuruga uchaguzi; aliwataka wabadilishwe.

“Tunajua maafisa wengi walioajiriwa kwa uchaguzi huu walikuwa wa jumuiya moja. Wanapaswa kubadilishwa. Tutazungumza haya wakati tume itatangaza tarehe mpya," alisema.

Awiti aliwataka wafuasi wake kuwa watulivu, akiongeza kuwa yuko tayari kupiga kura punde tu IEBC itakapotangaza tarehe mpya ya uchaguzi.

"Ninawaomba Wakenya kudumisha amani na utulivu, nchi ni yetu sote kwa hivyo hakuna haja ya kupigana," alisema.

“Kama kuna tatizo tufuate sheria, ndivyo tunavyojenga jamii imara,” alisema.

View Comments