In Summary

•Shughuli ya kuhesabu kura kwa sasa zinaendelea mara baada ya vituo vya kupiga kura kufungwa huku hesabu ya kura za urais ikipewa kipaumbele.

•Uchaguzi huu unaonekana kama utakuwa na kinyang'anyiro kikali kati ya wagombezi Bw Odinga, 77, na Bw Ruto, 55.

Wapiga kura walipanga foleni tangu mapema asubuhi katika vituo vya kupigia kura kote nchini Kenya
Image: AFP

Ucheleweshaji wa vifaa na changamoto za utambulisho katika baadhi ya maeneo ya kulitia doa nchi siku ya uchaguzi ambao ulikuwa wa amani kwa kiasi kikubwa nchini Kenya.

Shughuli ya kuhesabu kura kwa sasa zinaendelea mara baada ya vituo vya kupiga kura kufungwa huku hesabu ya kura za urais ikipewa kipaumbele.

Kura hii inafuatia kampeni kali iliyotawaliwa na mijadala kuhusu gharama za maisha, ukosefu wa ajira na ufisadi.

Wanaogombea wakuu wa urais ni aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga na Naibu Rais wa sasa William Ruto.

Wakenya pia walikuwa wakichagua bunge jipya na tawala za mitaa.

Tume ya uchaguzi bado haijatangaza jumla ya waliojitokeza kupiga kura, lakini kufikia saa kumi jioni (13:00 GMT) - saa moja kabla ya uchaguzi kufungwa - zaidi ya 56% ya wapiga kura milioni 22 waliojiandikisha walikuwa wamepiga kura zao.

Afisa mkuu wa uchaguzi mjini Nyeri katika eneo la kati nchini Kenya aliwaambia wanahabari kwamba waliojitokeza kupiga kura katika eneo hilo walikuwa wachache ikilinganishwa na uchaguzi wa mwaka 2017.

Awali Bw Odinga alilakiwa na wafuasi wake alipoenda kupiga kura katika eneo la Kibra - moja ya ngome zake katika mji mkuu, Nairobi.

Hakuzungumza na waandishi wa habari, lakini mkewe, Ida Odinga, alisema "amefurahishwa na uchaguzi".

Bw Ruto alipopiga kura katika mji wa Eldoret uliopo eneo la Bonde la Ufa aliahidi kukubali matokeo ya uchaguzi.

"Nadhani kwa mara ya kwanza katika historia ya demokrasia ya vyama vingi nchini Kenya, wagombea wote wamejitolea kukubali matokeo ya matokeo," aliambia BBC.

Mzozo kuhusu matokeo ya uchaguzi wa mwaka 2007 ulisababisha ghasia za wiki kadhaa na kusababisha vifo vya takriban watu 1,200 na kuwalazimu takriban watu 600,000 kuyakimbia makazi yao.

Siku ya Jumanne, kulikuwa na hali ya kufadhaika miongoni mwa wapiga kura asubuhi na mapema katika kituo cha kupigia kura katika shule ya msingi ya eneo la Westlands jijini Nairobi.

Walizuiwa kuingia katika eneo la shule kwa dakika 90.

Watu walikasirishwa na ucheleweshaji wa uchaguzi katika kituo kimoja cha kupigia kura katika mji mkuu, Nairobi

Kilichosababisha kucheleweshwa kwa shughuli hiyo hakikubainishwa lakini baadhi ya watu walianza kupiga mayowe wakisema: "Tunataka kupiga Kura!"

"Nilikuwa hapa mapema sana. Ni hali ya kukatisha tamaa kwamba tulifika hapa mapema na tulilazimika kusubiri kwa muda mrefu," mpiga kura Alex Kipchoge aliambia BBC.

Upigaji kura ulipoanza, hata hivyo, mchakato ulikwenda vizuri.

"Nilifurahi sana. Nimekuwa nikingojea hili kwa muda mrefu na nina furaha kwamba nimepata nafasi ya kupiga kura," mpiga kura wa mara ya kwanza Abigail Awili alisema.

Pia kulikuwa na ucheleweshaji katika eneo la pwani ya Mombasa na baadhi ya maeneo ya kaskazini-mashariki mwa nchi. Na katika sehemu za kaunti ya Kakamega, magharibi, baadhi ya vifaa vya kielektroniki vya kukagua alama za vidole vilishindwa kufanya kazi.

Lakini tume ya uchaguzi ilisema kuwa nchi nzima ni 200 pekee waliovunjika kati ya jumla ya zaidi ya 46,000.

Matokeo ya uchaguzi uliopita wa urais mwaka 2017 yalibatilishwa baada ya Mahakama ya Juu kutoa uamuzi kwamba tume ya uchaguzi haikufuata sheria lilipokuja suala la kuwasilisha matokeo kwa mfmo wa kielektroniki kutoka vituo vya kupigia kura.

Majaji waliamua kwamba "uvunjaji wa sheria na ukiukwaji" ulifanyika.

Uchaguzi wa marudio ulishindwa na Bw Kenyatta, lakini ukasusiwa na Bw Odinga - mgombea mkuu wa upinzani wakati huo.

Mwenyekiti wa tume ya uchaguzi Wafula Chebukati ambaye pia alikuwa msimamizi wa kura ya 2017 amejaribu mara kwa mara kuwahakikishia Wakenya kwamba timu yake itatekeleza jukumu hilo wakati huu.

Baba v Hustler

Uchaguzi huu unaonekana kama utakuwa na kinyang'anyiro kikali kati ya wagombezi Bw Odinga, 77, na Bw Ruto, 55.

Bw Odinga - kiongozi wa upinzani wa muda mrefu, anayeitwa ''Baba'' na wafuasi wake, anawania urais kwa mara ya tano. Bw Ruto, ambaye amejaribu kusisitiza uhusiano wake na Wakenya wa kawaida kwa kujiita "hustler", anawania kiti cha urais kwa mara ya kwanza.

Wagombea wengine wawili - David Mwaure na George Wajackoya - pia wako kwenye kinyang'anyiro hicho.

Ili kushinda uchaguzi wa urais katika duru ya kwanza, mgombea anahitaji:

  • zaidi ya nusu ya kura zote zilizopigwa kote nchini
  • angalau 25% ya kura zilizopigwa katika majimbo 24.

Baada ya kuhesabu kura, maafisa watapiga picha ya hesabu ya mwisho na kutuma picha hiyo kwa maeneo bunge na vituo vya kitaifa vya kujumlisha kura.

Ili kuhakikisha uwazi vyombo vya habari, vyama vya siasa na mashirika ya kiraia yamehimizwa kuendesha hesabu zao kwa kutumia matokeo ya mwisho yaliyotangazwa katika vituo zaidi ya 40,000 vya kupigia kura.

Lakini tume ya uchaguzi pekee ndiyo inayoweza kutangaza mshindi wa uchaguzi wa urais baada ya kuthibitisha fomu halisi na za kidijitali zinazotumwa kwa kituo cha kitaifa cha kuhesabia kura.

Ina siku saba kutangaza matokeo.

View Comments