Licha ya kutegemea watu wake kumpigia kura katika uchaguzi uliokamilika, mgombea urais wa Roots George Wajackoyah alipata kura 49 pekee katika kituo chake cha kupigia kura Matungulu, kaunti ya Kakamega.
Kulingana na matokeo ya tovuti ya IEBC, Wajackoyah alishindwa na mgombea urais wa Azimio Raila Odinga aliyepata kura 799.
DP William Ruto alipata kura 109 huku kiongozi wa chama cha Agano Waihiga Mwaure akipata kura mbili.
Kiongozi wa chama cha Roots alikuwa na tatizo la kupiga kura huku vifaa vya KIEMS vilishindwa.
Ilibidi maajenti hao wamtambue kwa mikono huku akidai kuwa mfumo huo ulikuwa unapanga kumtoa kwenye kinyang’anyiro cha urais.
Alisema mfumo huo ulilenga ngome yake Magharibi, ambapo kushindwa kwa vifaa vya KIEMS kulienea.
"Walianza kuonyesha kwamba nilikuwa na asilimia 15, wakahamia saba, kisha wakahamia tano na hatimaye asilimia mbili na sasa wananizuia kupiga kura," alisema.
Wajackoyah amekuwa akimpigia debe Raila, akisema alikuwa mmoja wa wakombozi waliokuwa wakileta mabadiliko.
Siku chache kabla ya uchaguzi mkuu, kulikuwa na madai kwamba Wajackoyah angemuunga mkono Raila kuwania urais.
Lakini alijitokeza na kukanusha madai hayo akisema alikuwa kwenye kinyang'anyiro cha kubaki.
Hii ilikuwa baada ya mgombea mwenza Justina Wamae kudai kuwa hakushauriwa iwapo chama kilimwidhinisha Raila. Wamae alisema kuwa ikiwa ndivyo, angemuunga mkono William Ruto wa UDA.
Tafsiri na MOSES SAGWE