In Summary

•Babu Owino wa ODM alichaguliwa tena na wapiga kura 65,540, akimshinda mpinzani wake wa UDA Francis Mureithi aliyepata kura 34,450.

•Wagombea wengine wa ODM ambao wameshinda kinyang’anyiro cha ubunge ni pamoja na George Aladwa (Makadara), Tom Kajwang’ (Ruaraka) na Antony Oluoch (Mathare).

Babu Owino, mbunge wa Embakasi East
Image: Babu Owino////Facebook

Muungano wa Azimio La Umoja unaoongozwa na Raila Odinga umeshinda viti 14 kati ya 17 vya ubunge katika kaunti ya Nairobi.

Ingawa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka bado haijatangaza rasmi washindi katika maeneo yote, wapinzani wengi wa wagombea tayari wamekubali kushindwa.

Phelix Odiwuor almaarufu Jalang'o (Lang'ata) wa ODM ni miongoni mwa waliochaguliwa.

Mbunge wa sasa Nixon Korir alikubali kushindwa Jumatano, akisema hesabu ilionyesha kuwa Jalang'o alikuwa ameongoza. Tim Wanyonyi wa ODM alipata kiti cha Westlands, huku mpinzani wake wa karibu wakili Nelson Havi akimpongeza.

"Sisi ni wachache katika kinyang'anyiro cha Westlands. Wengi walimchagua Timothy Wanyonyi. Wanastahili ipasavyo kwa busara zao au ukosefu wake. Kwa upande wetu, tumeridhika na matokeo. Hongera kwako kaka yangu mkubwa, Tim Wanyonyi. Tumikia vyema," Havi alitweet.

Katika eneo la Embakasi Mashariki, Babu Owino wa ODM alichaguliwa tena na wapiga kura 65,540, akimshinda mpinzani wake wa UDA Francis Mureithi aliyepata kura 34,450.

Mbunge wa sasa wa Embakasi Magharibi George Theuri pia alikubali kushindwa akikiri kuwa mpinzani wake wa Jubilee Mark Mwenje alikuwa amemshinda.

"Tunapoanza sura mpya, niruhusu nimtakie mshindani wangu anayestahili na mbunge anayekuja Mark Mureithi Mwenje kila la heri anapoanza enzi mpya kama mbunge mteule," Theuri alisema.

Kulingana na matokeo ya awali, wagombea wengine washirika wa Azimio ambao wameshinda ni Isaac Waihenya Ndirangu wa Roysambu (Jubilee), Beatrice Elachi wa Dagoretti Kaskazini (ODM), Amos Mwago wa Starehe (Jubilee) na Dennis Waweru wa Dagoretti Kusini (Jubilee).

Huko Kamukunji, Hassan Abdi anaongoza. Alikuwa akiwania kwa tiketi ya Jubilee. Mwalimu Peter Orero wa Kibra pia amejinyakulia kiti hicho kwa tiketi ya ODM.

Wagombea wengine wa ODM ambao wameshinda kinyang’anyiro cha ubunge ni pamoja na George Aladwa (Makadara), Tom Kajwang’ (Ruaraka) na Antony Oluoch (Mathare).

Huko Embakasi Kusini, Julius Mawathe wa Wiper amenyakua kiti hicho tena.

Huko Kasarani, Ronald Karauri, mgombeaji huru, aliibuka mshindi.

Mwaniaji wa Jubilee ya Embakasi ya Kati Samuel Mwangi alikubali kushindwa na mpinzani wake wa UDA Benjamin Gathiru, ambaye pia ni mbunge wa sasa.

Mwendo wa saa tano usiku wa Jumatano, Gathiru alikuwa akiongoza kwa kura 7,000 dhidi ya kura 4,000 za Mwangi.

Matokeo hayo yalitoka katika vituo 89 kati ya 215 vilivyokuwa vimewasilisha matokeo yao wakati wa kuchapishwa.

Radio Jambo bado haijabaini matokeo katika eneo bunge la Embakasi Kaskazini.

View Comments