In Summary

•Wasimamizi wawili wa uchaguzi wametiwa mbaroni na maafisa wa polisi kwa madai ya kuhusika na makosa ya uchaguzi katika taasisi ya KSG.

•Mgombea ubunge Hassan Mwanyoha alisema hawana imani tena na zoezi hilo kwani lilikumbwa na dhuluma tangu siku ya kwanza.

Kamanda wa Polisi wa Kaunti alituliza watahiniwa katika kituo cha kuhesabia kura cha Matuga KSG huko Kwale Jumatano, Agosti 11, 2022.
Image: SHABAN OMAR

Wasimamizi wawili wa uchaguzi wametiwa mbaroni na maafisa wa polisi kwa madai ya kuhusika na makosa ya uchaguzi katika taasisi ya Kenya School of Government katika kaunti ndogo ya Matuga.

Wawili hao walitoka katika vituo vya kupigia kura vya Vuga primary.

Walikamatwa baada ya kushutumiwa kwa kupanga njama ya kubadilisha matokeo ya jumla ya kura.

Kulingana na vyanzo vya habari, wawili hao walipatikana wakiwa na vifaa vya kupigia kura na vya KIEMS nyuma ya kituo rasmi cha kuhesabia kura.

Polisi waliokuwa wakisimamia eneo hilo walijibu upesi na kuwakamata wawili hao kufuatia malalamishi ya baadhi ya wagombea.

Wagombea walikuwa wamekosa subira na kulazimisha shughuli za kujumlisha kura zisitishwe.

Mgombea wa kiti cha Ubunge wa Matuga, Hassan Mwanyoha alidai kuwa mchakato mzima wa upigaji kura uligubikwa na dhuluma iliyohitaji kusitishwa hadi hatua nyingine za kisheria zitakapochukuliwa.

Wakati akizungumza na kamanda wa polisi wa kaunti ya Kwale Josphat Kinyua ambaye alikuwa ameingilia kati, Mwanyoha alisema hawana imani tena na zoezi hilo kwani lilikumbwa na dhuluma tangu siku ya kwanza.

"Wasimamizi wa uchaguzi walikuwa wakiwazuia maajenti kuingia kwenye vituo vya kupigia kura na kushuhudia zoezi la upigaji kura. Hapo ndipo mchezo mzima ulipoanzia," alisema.

Hata hivyo, Kinyua alihoji ni kwa nini Mwanyoha hakuwasilisha malalamishi yake mapema vya kutosha.

Mgombea wa useneta wa Kwale Salim Mwadumbo alisema kuna visa kadhaa ambapo masanduku ya kura hayakufungwa na kuhatarisha zoezi la uchaguzi.

Alisema baadhi ya maajenti walinyimwa fursa ya kuhakiki fomu 34A na hivyo kuibua mashaka kuhusu uaminifu wa uchaguzi huo.

“IEBS inaonekana kuathiriwa kwa sababu tumewasilisha malalamishi yetu mengi lakini hakuna hatua zilizochukuliwa kufikia sasa,” alisema.

Mwadumbo alisema wao kama wagombea hawatakubali matokeo hadi suala hilo litatuliwe ipasavyo.

Msimamizi wa uchaguzi wa Jimbo la Matuga Abdallah Chikophe alikiri kupokea malalamiko kuwa baadhi ya wasimamizi walikuwa wakivuruga baadhi ya matokeo.

Chikophe alisema hatua stahiki zilichukuliwa lakini maajenti na walalamikaji hawakuweza kuthibitisha tuhuma zao.

Alisema wanaamua kutatua suala hilo lakini walalamikaji hawakuwa na ushirikiano na walizidisha suala hilo.

“Ni kweli msimamizi alikutwa nje ya kituo cha kujumlisha kura akiwa na fomu 34As ambayo ilitolewa kidogo kwenye bahasha lakini haikuwa imeharibiwa na niliwauliza maajenti kama tunaweza kuthibitisha kwenye mfumo lakini walikataa,” alisema.

Chikophe alisema hayo walipojaribu kukabiliana na maafisa wasimamizi ambao mmoja wao alikuwa na vifaa vya KIEMs.

Alisema kwa sababu ya kutoelewana kuliibuka machafuko na ndipo alipoamua kupiga simu polisi.

Wakati huo huo, Kinyua alisema washukiwa hao wawili wako chini ya ulinzi wa polisi kwa mahojiano.

Hata hivyo, alisema zoezi la upigaji kura bado ni la kuaminika na kuna uwazi ili kuhakikisha uchaguzi huru na wa haki

View Comments