logo

NOW ON AIR

Listen in Live

Baadhi ya ‘sababu za Ruto kumshinda Raila katika uchaguzi wa urais’

Chebukati alisema alimtangaza Bw Ruto kuwa Rais Mteule ''kulingana na katiba na sheria''.

image
na Samuel Maina

Uchaguzi19 August 2022 - 11:48

Muhtasari


    Naibu Rais wa Kenya William Ruto ametangazwa kuwa ndiye Rais Mteule Kenya kufuatia ushindani mkali baina yake na Waziri mkuu wa zamani Raila Odinga.

    Bw Ruto amefanikiwa kupata ushindi wa 50.49%, ya kura , huku mshindani wake na kiongozi wa upinzani wa muda mrefu Bw Odinga, akipata 48.8% ya kura, kulingana na matokeo rasmi yaliyotangazwa na mwenyekiti wa Tume ya taifa ya uchaguzi (IEBC)- matokeo ambayo upande wa Bw Odinga wameyapinga. Makamishna wanne kati ya saba wa tume ya IEBC pia wametofautiana na matokeo hayo.

    Hatahivyo Mwenyekiti wa tume ya uchaguzi, Wafula Chebukati amesema amemtangaza Bw Ruto kuwa Rais Mteule ''kulingana na katiba na sheria''.

    'Ushindi ambao haukutarajiwa na wengi'

    Ushindi wa Bw.Ruto dhidi ya mpinzani Raila Odinga, haukutarajiwa na baadhi ya Wakenya wengi hususan kutokana na kutofautiana na mkuu wake rais anayeondoka mamlakani Uhuru Kenyatta , ambaye aliamua kumuunga mkono Bw Odinga - hasimu wake wa zamani katika uchaguzi wa tarehe 9 Agosti 2022.

    Licha ya kwamba Odinga na Ruto hawatoki katika kabila kubwa zaidi nchini Kenya la Wakikuyu 2, baadhi ya Wakenya waliamini kuwa huenda Wakikuyu wengi wangempigia kura Bw Odinga kwasababu aliungwa mkono na Bw Kenyatta ambaye ni Mkikuyu na ambaye aliaminiwa kuwa na ushawishi miongoni mwa watu wa kabila lake. Hata hivyo matokeo ya uchaguzi yalionekana kinyume na hilo.

    Lakini je ni mambo gani hasa yaliyomfanya Bw William Ruto kupata ushindi dhidi ya Raila Odinga?

    Kampeni ya mapema

    Mkakati wa Bw William Ruto wa kuanza kampeni ya kuwania urais takriban miaka mitatu baada ya uhusiano wake na Uhuru kuvunjika kufuatia makubaliano baina ya Rais Kenyatta na Bw Odinga unaonekana kuwa mojawapo ya sababu zilizochangia pakubwa ushindi wake. Wakati Bw Odinga alipokuwa akishirikiana na Rais Kenyatta kunadi mafanikio ya Uhuru serikali ya Kenyatta, Ruto alikuwa tayari ameanza kampeni za uchaguzi na kuweka wazi kasoro za serikali alizozihusisha na muungano mpya wa mkuu wake na Raila Odinga uliofahamika kama ''Handshake'' .

    Kampeni za mapema za kuwania urais mwaka 2022 alizofanya Bw william Ruto zinaaminiwa kumsaidia kuweza kuwarai wapiga kura mapema kwa sera zake

    Alifanikiwa katika kuyaanika maovu ya serikali ya Rais Uhuru Kenyatta kwa umma wa Wakenya, ni dhahiri kwamba sehemu kubwa ya wapiga kura wameonyesha kuwa wanakubaliana naye kwa hilo.

    Turufu ya Mtafutaji dhidi ya warithi wa mamlaka

    Katika kampeni za chaguzi Bw Ruto alijita "hustler", au ''mtafutaji, huku akiwashutumu mahasimu wake wawili kuwa ''dynasties'' au watu wanaotaka kuendeleza utawala wa kurithishana - wa familia za Kenyatta na Odinga. Kwa kutumia turufu hiyo Bw Ruto alituma ujumbe kwa Wakenya kwamba ''hata Mkenya wa kawaida anaweza kuongoza nchi sio uongozi lazima utoke kwa familia Tajiri pekee'', ujumbe ambao alikuwa aliutoa mara nyingi katika kampeni yake.

    Katika kampeni za uchaguzi kuwania urais Bw Ruto alitumia mkokoteni kama kielelezo cha watafutaji atakaowasaidia kuinua maisha yao, iwapo atachaguliwa kuwa rais

    Aliwavutia vijana hususan vijana kutoka familia zenye kipato cha chini kuamini kuwa huenda anaweza kuelewa matatizo hususan ya kiuchumi na kuyapatia ufumbuzi.

    Neno ''hustlers'' nchini Kenya linamaanisha -hasa vijana - wanaohangaika kujitafutia riziki katika hali hali ngumu ya uchumi Kwa hilo alivutia hisia za huruma kwa Wakenya kwa maombi, kuangua kilio, na kudai kuwa Rais uhuru Kenyatta anamtishia.

    'Muungano na wanasiasa wenye ushawishi'

    Hatua ya Bw Ruto kuunda muungano wa kisasa (Kenya Kwanza Alliance) na wanasiasa maarufu kama vile Moses Wetangula na Musalia Mudavadi ni mbinu ambayo imemsaidia Bw Ruto kuweza kuwavutia wapiga kura zaidi kutoka maeneo ambayo awali hayakuwa ngome yake. Wanasiasa hawa ambao wanatoka katika eneo la magharibi mwa Kenya wameweza kumpatia kura nyingi kuliko walizopata yeye na Uhuru Kenyatta katika uchaguzi wa mwaka 2007.

    Kwa upande mwingine Bw Raila Odinga alipoteza kura nyingi hususan ni katika ngome ya mgombea kiongozi wa kisiasa wa Amani National Congress, Musalia Mudavadi eneo ambalo awali lilifahamika kama ngome yake katika ucgaguzi wa miaka uliopita, .

    Kura kutoka makabila yenye idadi kubwa wapiga kura

    Bila shaka Bw Ruto atakumbukwa kwa kuweza kupenya katika jamii yenye idadi kubwa ya wapiga kura la Wakikuyu na kujizolea kura kuliko mpinzani wake Raila Odinga. Sio jambo lililotarajiwa na baadhi ya Wakenya kwamba Bw Ruto angeweza kumpiku Rais Uhuru Kenyatta kwa kura zaidi za watu wa kabila lake. Binafsi Kenyatta anatoka katika kabila la Wakikuyu na hivyo ilitegemewa kwamba kwa kumkampenia Raila Odinga katika Mlima Kenya angeweza kumsaidia swahiba wake Odinga kuingia Ikulu, jambo ambalo halikuwezekana.

    Katika Muungano wake wa United democratic Alliance, Ruto aliwajumuisha wanasiasa kutoka jamii za Mlima Kenya na kutoka kabila la kela Kalenjin ambao walimsaidia kuvuna kura kutoka maeneo yake na kuendeza ajenda zake za kisiasa hususan ajenda ya kukuza uchumi kutoka chini kwenda juu.

    Baadhi ya wachambuzi nchini Kenya wanasema, Odinga na Kenyatta huenda walidhani kuwa wangepata kura za Mlima Kenya kirahisi kutokana na ''ushawishi'' wa Bw Kenyatta katika eneo hilo, na hivyo kutoendesha kampeni za mapema kama hasimu wao, jambo ambalo limedhihirika kuwa kinyume.

    Ruto tayari alikuwa na ushawishi mkubwa kutoka katika kabila lake la Kalenjin ambalo lilimpingia kura kwa wingi, katika uchaguzi uliopita.

    Suala la Bw Raila kuungwa mkono na Rais Kenyatta pia limeonekana na wafuasi wake kama ''laana'' badala ya ''neema'', kutokana na kile kinachoonekana ghadhabu ya wakazi wa Mlima Kenya hususan wafanyabiashara wadogo wanaomlaumu Rais Kenyatta kushindwa kuinua biashara yao, na kuyafanya maisha yao kuwa magumu.

    Katika kampeni zake pia Ruto alimlaumu Bw Kenyatta kwa kushindwa kutekeleza ajenda kuu nne, ambazo zingeweza kusaidia kuinua uchumi, kutokana na ''Handshake'', na Raila Odinga.

    'Mcha Mungu sugu'

    Nchini kenya inakadiriwa kuwa 85% ya watu ni Wakristo, kulingana na makadirio ya serikali yam waka 2019. Bila shaka Bw Ruto alifahamu kuwa nasingeweza kuikonga mioyo ya wapiga kura wakristo bila kuonekana kama ''mcha Mungu' na Mwanamaombi sugu , ambaye anamtegemea Mungu kwa yote. Kuanzia kutoa michango ya fedha kwa ajili ya ujenzi wa makanisa, kusaidia waumini wasiojiweza na kutaja Jina ''Mungu'', mara kwa mara, bila shaka ni jambo lililomsaidia sana Bw Ruto kujihusisha na wapiga kura Wakristo kuhisi ni mgombea anayewafaa.

    Uwepo wake makanisani na kujihusisha na viongozi wa kidini kulimfanya Bw Ruto kuonekana kama mtu mnyenyekevu, licha ya shutuma za ufisadi kutoka kwa mahasimu wake wa kisiasa akiwemo Bw Raila Odinga.

    Wakati Ruto alipokuwa akiendesha kampeni zake makanisani na kutoa michango mikubwa ya pesa huko, Raila Odinga alimshutumu kutumia pesa za wananchi alizopora kwa ufisadi kutoa misaada kwa makanisani, bila ushahidi.

    'Kuvunjika kwa ndoa yake na Uhuru Kenyatta '

    Suala la kuvunjika kwa kile kilichofahamika kama ''ndoa'', (Muungano wa Uhuru na Ruto) suala lilowakanganya Wakenya waliouunga mkono Muungano na serikali yao ya Jubilee hususan kutoka jamii za Wakikuyu na Wakalenjin, huku baadhi walimlaumu Bw Kenyatta kwa kumsaliti Bw Ruto, ambaye kwa mujibu wa makubaliano baina yao, Kenyatta angemuunga mkono Ruto katika nia yake ya kuwa rais, lakini hakufanya hivyo.


    RADIO JAMBO FREQUENCIES

    Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


    logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved