In Summary

•Nassir ambaye alihudumu kama mbunge katika eneo bunge la Mvita kwa miaka 10 alipata kura 24,406 katika eneo hilo ilhali mgombea wa upinzani Omar alikuwa na kura 19,086.

•Katika kaunti ya Kakamega, chama cha ODM pia kilitwaa uongozi wa ugavana huku Fernades Barasa ambaye ni mgombeaji wao akiongoza pia

Gvana mteule wa Mombasa, Nassir Shariff
Image: MAKTABA

Mgombea wa ODM Abdulswamad Nassir anatazamia kutangazwa gavana wa Mombasa baada ya kupata kura 119,083 katika uchaguzi wa Jumatatu.

Mpinzani wake mkuu, Hassan Omar wa UDA alipata kura 98, 108.

Matokeo bado hayajatangazwa rasmi na  Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kwani mchakato wa kujumlisha na uhakiki bado unaendelea katika Shule ya Serikali ya Kenya, Mombasa.

Kulingana na matokeo yaliyotolewa na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), Nassir alikuwa anaongoza katika maeneo bunge ya Jomvu, Changamwe, Nyali, Mvita, Likoni na Kisauni.

Katika eneo bunge la Jomvu, Nassir alikuwa na kura 15,629 huku Hassan Omar akiwa na kura 11,038.

Katika eneo bunge la Changamwe, Nassir alikuwa na kura 17,740 dhidi ya mshindani wake Omar ambaye alikuwa na kura 15,898.

Nassir ambaye alihudumu kama mbunge katika eneo bunge la Mvita kwa miaka 10 alipata kura 24,406 katika eneo hilo ilhali mgombea wa upinzani Omar alikuwa na kura 19,086.

Katika Jimbo la Nyali, kulikuwa na tofauti ya kura 807 pekee ambapo Nassir alikuwa na jumla ya kura 22,387 na Omar kura 21,580.

Katika eneo la Likoni ambako inajulikana kama eneo la ODM, Nassir alikuwa na 17,425 dhidi ya mshindani wake Omar ambaye alikuwa na kura 9,756.

Huko Kisauni, Nassir alipata kura 21,270 dhidi ya 20,750 za Omar.

Jana usiku, sherehe zilikuwa eneo la biashara la Mombasa ya Kati baada ya kubainika kuwa mgombeaji wa ugavana wa ODM Nassir anaongoza katika vituo vingi vya kupigia kura.

Mbunge wa Jomvu aliyechaguliwa chini ya ODM Badi Twalib ambaye alikuwa miongoni mwa watu wanaompongeza mgombeaji wa chama hicho alisema kuwa Nassir ni kiongozi mwenye maono na mtu makini ambaye wanaamini ataifanyia Mombasa kaunti kazi vizuri.

“Nassir ni kiongozi ambaye mimi binafsi nikiwa mbunge wa Jomvu nimefanya naye kazi kwa miaka 10 kwenye Bunge la Kitaifa na amekuwa karibu nasi. Mombasa ni eneo la ODM ambapo viongozi wote kuanzia mimi kama mbunge, seneta na mwakilishi wa wanawake ambao ni wanachama wa ODM,Tulitabiri ushindi wake kama gavana mteule ajaye na leo tunashukuru kwa sababu umetimia," alisema Twalib.

Aliongeza kuwa chama hicho kina wafuasi wa kutosha na kwamba hawakutetereka na matokeo ambayo yalitangazwa na tume ya uchaguzi baada ya uchaguzi mkuu.

Katika kaunti ya Kakamega, chama cha ODM pia kilitwaa uongozi wa ugavana huku Fernades Barasa ambaye ni mgombeaji wao akiongoza pia.

"Ninataka kusema kwamba hii ni onyo la kuwaambia wale wanaopanga kuiba kura za kiongozi wa chama chetu Raila Odinga kujua kwamba ana wafuasi wa kutosha," aliongezea.  

Twalib ambaye alikuwa kinara wa timu ya ODM katika kinyang'anyiro cha ugavana Mombasa alisema walifanya kazi pamoja kama timu kuhakikisha kuwa uchaguzi hiyo imekuwa sawa na kuhakikisha kuwa wameshinda Kakamega na Mombasa.

Mbunge huyo ambaye anaenda kuhudumu eneo bunge la Jomvu kwa wakati huo alimpongeza Hassan Joho kwa kuhudumu Mombasa kwa miaka 10 kama gavana.

"Nimefanya kazi na Joho kwa miaka 10, ataondoka ofisini kama gavana na kumtengenezea njia gavana mpya ambaye ni Nassir ili tushirikiane kuipeleka Mombasa katika ngazi ya juu zaidi," Twalib alisema.

Alisema uchawi aliotumia Nassir kushinda uchaguzi huo ni kuuza sera ambayo yalilenga ajenda ya maendeleo kwa watu.

Gavana wa Mombasa anayeondoka Hassan Joho na Nassir pia waliwaongoza wafuasi wa ODM katika kusherehekea kuzunguka mitaa ya Mombasa jana usiku ambapo maelfu ya wafuasi walikusanyika katika eneo la Treasury Square karibu kusherehekea.

 

View Comments