In Summary

• Wagombea wote waliahidi kwamba katika siku 100 wangeweza kukabiliana na swala nyeti la kiuchumi mbali na jinamizi la Ufisadi.

• Walishindwa kuelezea ni wapi mabilioni ya fedha wanazozungumzia zitapatikana ili kutekeleza mapendekezo yao. 

William Ruto

Kufuatia hatua ya mahakama ya juu kumuidhinisha William Samoei Ruto kuwa rais mteule wa Kenya ,Wakenya wengi sasa wanasubiri kuapishwa kwake ili kupata fursa ya kuwahudumia.

Uchaguzi wake unajiri wakati ambapo Wakenya wanakumbwa na hali mbaya ya kiuchumi iliyosababishwa na janga la Corona mbali na vita vinavyoendelea nchini Ukraine

Hatahivyo wakati wa kampeni wagombea wote wa urais walitoa ahadi zao kedekede kwa Wakenya kutatua tatizo hilo.

Wagombea wote waliahidi kwamba katika siku 100 wangeweza kukabiliana na swala nyeti la kiuchumi mbali na jinamizi la Ufisadi , mawazo yaliowavutia wapiga kura wengi.

Hatahivyo wengi wao walishindwa kuelezea ni kwa jinsi gani wangeweza kupitisha mapendekezo yao ambayo yanahitaji kuidhinishwa bungeni ili kuanza kutekelezwa.

Vilevile walishindwa kuelezea ni wapi mabilioni ya fedha wanazozungumzia zitapatikana ili kutekeleza mapendekezo ambayo yanalenga makundi maalum kutoka kwenye bajeti ya taifa ambayo tayari inakabiliwa na matatizo.

Kampuni inayotengeneza barakoa Kenya
Image: GETTY IMAGES

Ahadi za Rais Mteule William Ruto katika siku 100 za kwanza za utawala wake

Rais mteule William Ruto alipendekeza suluhu kwa matatizo yanayowakumba vijana , wanawake, wafanyabiashara wadogo wadogo mbali na kuweka vichocheo ambavyo vingetoa motisha kwa viwanda na kilimo mbali na vichocheo vingine vya kiuchumi.

Bei ya Unga

Wakenya wamekuwa wakipitia hali ngumu wakati huu wa mfumuko wa bei ambapo bei za bidhaa muhimu kama vile unga wa mahindi unaotumika aghalabu katika kila nyumba umepanda hadi kufikia ksh 200. Chakula kinachangia asilimia 54 ya matumizi ya kila nyumba, lakini Wakenya wanatumia asilimia 60 au zaidi. Tija ya kilimo haijaendana na ukuaji wa idadi ya watu, na hivyo kusababisha utegemezi mkubwa wa chakula kutoka nje. Katika ahadi yake rais Mteule aliapa kupunguza bei ya Unga kupitia ruzuku katika bei ya mbolea hali itakayosaidia kupungua kwa bei ya mahindi huku uzalishaji wa bidhaa hiyo pia ikuongezeka.

Hazina ya 'Hustlers'

Katika siku zake 100 za kwanza madarakani, Ruto aliahidi kuanzisha Hazina ya Hustlers ya shilingi bilioni 50, kutenga asilimia 50 ya Baraza lake la Mawaziri kwa wanawake, kutekeleza sheria ya uwakilishi wa theluthi mbili ya kijinsia kwa maafisa watakaoteuliwa na kuchaguliwa, na kusitisha uchunguzi unaodaiwa kuwa wa kuwalenga watu binafsi mbali na kukabiliana na ufisadi.

Uteuzi wa afisi ya waziri mkuu na kumpatia majukumu naibu wake

Vilevile ana mpango wa kumpatia majukumu naibu wake wa rais mbali na kubuni wizara ya Waziri mkuu ambayo pia amepanga kuipatia majukumu, kuanzisha wakala wa haki za wanawake katika ofisi ya rais na kuondoa vikwazo vya bima ya afya.

Fedha za kenya
Image: AFP

Kutenga fedha za mikataba ya kiuchumi katika kaunti 47

Pia atatenga fedha kwa kaunti zote 47 kwa ajili ya utekelezaji wa mikataba ya kiuchumi, na kuwateua majaji sita walioteuliwa ambao Rais Uhuru Kenyatta aliwakataa na hivyo kusababisha migogoro kati yake na Jaji Mkuu Martha Koome na mtangulizi wake David Maraga.

Sheria ya thuluthi mbili ya Kijinsia

Utekelezaji wa hitaji la kikatiba kwamba angalau theluthi mbili ya maafisa waliochaguliwa na kuteuliwa wawe wa jinsia tofauti limekuwa jambo la kuzingatia tangu sheria mpya kuu ilipotangazwa mwaka wa 2010.Ugumu wake haswa umekuwa upatanisho wa sheria ya kuhakikisha uwakilishi sawa wa wanawake katika Bunge.

''Kuna wanaosema kuwa haiwezekani kutekeleza sheria ya kijinsia ya thuluthi mbili. Nitahitaji tu siku 90 ofisini kuwa nayo na siku 180 kuijumuisha kikamilifu katika bodi nzima," DP alinukuliwa akisema na gazeti la Nation.

"Wanawake watakuwa na kamishna ambaye atawaongoza katika uwekezaji, urithi na ufuatiliaji wa haki zao kuanzia ngazi ya chini. Pedi zitatolewa bila malipo kwa wasichana wote wa shule, huku akina mama vijana wakifadhiliwa ili kutimiza ndoto zao."

Kutenga ksh. Bilioni 30 kuwasaidia wakulima

Ruto vilevile anasema atatenga Sh30 bilioni kuinua wakulima wadogo milioni mbili kwa kuwapa Sh15,000 kila mmoja kama ruzuku ili kupata uhakika wa chakula.

Bei ya bidhaa za kilimo zimepanda maradufu
Image: AFP

Ahadi nyingine ambazo ameahidi Wakenya ni pamoja na

  • Kuwekeza angalau Sh250 bilioni katika miaka mitano kuanzia 2023 ili kuimarisha Kilimo na usalama wa chakula
  • Kutoa Sh50b kila mwaka ili kuwapatia Wafanyabiashara wakubwa fursa ya kupata mkopo kwa uhakika
  • Kujenga nyumba mpya na za bei nafuu 250,000 kila mwaka kupitia ushirikiano wa sekta ya umma na binafsi
  • Kuanzisha hazina ya makazi ili kupata ardhi na kuwapa makazi hadi familia milioni moja zisizo na ardhi
  • Kufanya Hazina ya Kitaifa ya Bima ya Hospitali (NHIF) iwafikie Wakenya wote, ikiwa ni pamoja na kulipia michango ya wale ambao hawawezi kumudu malipo.
  • Kuanzishwa kwa hospitali mpya za kiwango cha 6 katika maeneo sita mapya na kuajiri wahudumu wa afya 20,000 wa awali.
  • Kuunda mtandao wa muunganisho wa fiber optic wa kilomita 100,000
  • Kuziba pengo la sasa la uhaba wa walimu ndani ya miaka miwili ya fedha
  • Kuongeza maradufu kiasi cha fedha kilichotengwa kwa ajili ya programu ya kulisha shuleni
  • Maafisa wa kada ya chini (sajenti na walio chini) kupewa chaguo la kuhudumu katika kaunti zao za nyumbani kuanzia umri wa miaka 50
View Comments