In Summary

•IEBC ilishutumu timu ya wanasheria ya Muungano wa Azimio kwa kuwasilisha kumbukumbu bandia yaani ‘fake logs’ baada ya uchunguzi wa tovuti ya umma.

•‘’Ufikiaji wa seva iliwezeshwa. Mawakala walipewa ufikiaji uliosimamiwa wa seva,’’ IEBC ilisema.

Jaji Mkuu Martha Koome
Image: BBC

Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka nchini Kenya siku ya Ijumaa, ilishutumu timu ya wanasheria ya Muungano wa Azimio kwa kuwasilisha kumbukumbu bandia yaani ‘fake logs’ baada ya uchunguzi wa tovuti ya umma.

Wakili Phillip Murgor alikuwa ameonyesha mahakama kile alichodai kuwa ni kumbukumbu kutoka kwa seva ya IEBC ambayo ilionyesha kuwa raia wa kigeni kadhaa walikuwa wametumia mfumo huo siku kadhaa kabla na baada ya uchaguzi.

Hata hivyo, Wakili Dennis Nkarichia wa IEBC alidai kuwa kumbukumbu hizo hazikuwa sehemu ya ripoti ya uchunguzi iliyowasilishwa mahakamani na msajili.

Hii ilisababisha Jaji Isaac Lenaola mwishoni mwa mawasilisho kumtaka Murgor kwenda kwenye ukurasa wa msajili ambao ulionyesha kuwa raia wa kigeni waliingilia uchaguzi kabla ya siku ya uchaguzi na si baada kama timu ya Azimio ilivyodai.

Kisha Murgor akafafanua mahakamani kwamba ripoti aliyowasilisha si ile ya mahakama bali ni kumbukumbu zao wenyewe ambazo alidai pia walizipata kutoka IEBC.

Upande wa IEBC ulisema kuwa:

‘’Ufikiaji wa seva iliwezeshwa. Mawakala walipewa ufikiaji uliosimamiwa wa seva,’’ ilisema.

Wakili wa IEBC Dennis Nkarichia, pia aliongeza kuwa ukaguzi wa kumbukumbu za ufikiaji seva haukuonyesha shughuli zozote za kutiliwa shaka kulingana na ripoti ya msajili wa Mahakama ya Juu.

Hapo jana timu yake ya wanasheria iliruhusiwa kuwasilisha ushahidi mpya kuonyesha kwamba matokeo ya mwisho ya uchaguzi ya Tume ya IEBC yalikuwa na dosari.

Katika matangazo ya moja kwa moja wakionyesha kwa majaji wa Mahakama ya Juu, mawakili wa Bw. Odinga walidai kuwa kifaa kimoja cha kuwatambua wapigakura kilitumiwa kutuma matokeo kutoka kwa vituo viwili vya kupigia kura vilivyo umbali wa mamia ya kilomita.

Mawakili wake pia waliwaonyesha majaji kile walichosisitiza kuwa makosa ya hesabu katika baadhi ya vituo vya kupigia kura, wakisema kuwa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) ilitumia takwimu bandia kumtangaza William Ruto kuwa rais mteule.

Mawasilisho hayo yalitolewa huku timu ya Bw Odinga ikiteta kwamba ukiukaji wowote wa katiba ni msingi tosha kwa Mahakama ya Juu kubatilisha uchaguzi.

Wakati huohuo, timu ya Muungano wa Azimio imejipata kwenye utata kwa kudaiwa kutoa ushahidi wa uwongo na Tume ya IEBC.

View Comments