logo

NOW ON AIR

Listen in Live

Kalonzo kujiunga na Kenya Kwanza?- Hatimaye aweka mambo wazi

Kumekuwa na tetesi kuwa kiongozi huyo wa Wiper anafanya mazungumzo na Ruto kuhusu jinsi atakavyoshirikishwa Kenya Kwanza.

image
na Samuel Maina

Uchaguzi21 August 2022 - 12:06

Muhtasari


  • •Kalonzo Musyoka amepuuzilia mbali madai ya kuugura muungano wa Azimio One Kenya na kujiunga na Kenya Kwanza.
  • •Jumamosi Kalonzo alijumuika na familia ya Raila kuwapokea viongozi wa dini na madhebehu mbalimbali waliomtembea Karen.
Naibu Rais William Ruto akiwa na kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka katika majengo ya Bunge wakati wa kutazamwa kwa mwili wa Rais mstaafu Mwai Kibaki.

Kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka amepuuzilia mbali madai ya kuugura muungano wa Azimio One Kenya na kujiunga na Kenya Kwanza.

Katika kipindi cha siku chache zilizopita kumekuwa na tetesi kuwa makamu huyo wa rais wa zamani anafanya mazungumzo na rais mteule William Ruto kuhusu jinsi atakavyoshirikishwa katika muungano huo ambao anaongoza.

Kalonzo hata hivyo amebainisha kuwa uvumi huo hauna msingi  na kuweka wazi kwamba kwa sasa anashirikiana na wenzake katika Azimio kupinga matokeo ya urais yaliyotangazwa na IEBC katika mahakama ya juu.

"Nadhani hao ni watu wenye matamanio. Mnajua tunakokwenda. Tunaenda moja kwa moja kuwafuata katika Mahakama ya Juu," Kalonzo aliambia NTV.

Katika siku chache zilizopita, kiongozi wa Kenya Kwanza na rais mteule William Ruto amekuwa akiwapokea baadhi ya wanasiasa kutoka muungano pinzani wa Azimio.

Kumekuwa na fununu kuwa naibu rais huyo anayeondoka yupo mbioni kuimarisha ushawishi wake nchini kwa kumsajili Kalonzo, madai ambayo kiongozi huyo wa Wiper ameyakana sasa.

Jumamosi Kalonzo alijumuika na familia ya Raila kuwapokea viongozi wa dini na madhebehu mbalimbali ambao walitembea nyumbani kwake Karen.

Katika mkutano huo, Raila aliwahakikishia wafuasi wake kuwa bado timu yake bado haijatupilia mbali azma ya kutwaa uongozi wa nchi kuwafahamisha kuwa wanatazamia kutafuta suluhu kwa njia ya amani.

"Sisi tumesema tunataka kuona kama haki itatendeka ndio amani ipatikane. Kama vile marehemu Desmond Tutu alisema, bila ukweli hakuwezi kuwa na amani. Vile vile bila amani hakuwezi kuwa na upatanisho," Alisema.

Alisema kuna Wakenya wengi ambao bado wameshtuka kutokana na matokeo yaliyotangazwa Jumatatu  ilhali wengine wanasherehekea.

"Tumesema sisi hatutaki kuona fujo au vurugu katika nchi yetu. Tunataka kuona amani ikidumu na ndio sababu tumeamua kutumia sheria na kuenda mbele ya mahakama kuu ili tupeleke ushahidi ambao tuko nao kuonyesha kuwa ilikuwa mzaha ya uchaguzi. Nafanya hii kutetea demokrasia ya taifa letu," Alisema.

Jumatatu, mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka Wafula Chebukati Jumatatu alimtangaza William Ruto kuwa rais mteule baada ya kuzoa  kura 7,176,141 huku Raila akipata kura 6,942,930.

Raila hata hivyo alidai kuwa tangazo la Ruto kama rais mteule lilikuwa batili.


RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved