In Summary

•Ruto amedokeza kuwa watumishi wa umma wanalazimishwa na kutishiwa kuharibu na kuhujumu uchaguzi mkuu.

•Naibu rais alidokeza ugomvi zaidi wa ndani kati yake na rais Kenyatta huku akimuomba asidhuru watoto wake.

Naibu rais na kiongozi wa Kenya Kwanza
Image: William Samoei Ruto (Facebook)

Mgombea urais wa Kenya Kwanza William Ruto amemshutumu Rais Uhuru Kenyatta kwa kupanga kuvuruga uchaguzi mkuu ujao.

Ruto amedokeza kuwa watumishi wa umma wanalazimishwa na kutishiwa kuharibu na kuhujumu uchaguzi wa mwezi ujao.

"Mheshimiwa Rais, kwa nini machifu na watumishi wengine wa umma wanalazimishwa na kutishiwa kwenye mikutano ya siri ili kupuuza, kuchezea na kuhujumu chaguzi za amani? Itakunufaisha nini kuanzisha mizozo miongoni mwa Wakenya wasio na hatia?" Ruto alimhoji rais kupitia Facebook.

Kufuatia madai hayo, naibu rais amemtaka rais Kenyatta kukoma huku akidokeza kuwa mwelekeo huo huenda ukazamisha nchi.

"Bosi, tusiipeleke nchi upande huu!" Alisema.

Ujumbe huo ulijiri masaa machache tu baada ya Ruto kumfokea kiongozi wa taifa akimshtumu kwa  kutishia maisha yake.

Akizungumza mjini Kapsabet Ijumaa, naibu rais alimrai bosi wake kudumisha heshima kati yao na kumuomba amuache peke yake.

Ruto alimwambia rais kuwa hahitaji uungwaji mkono na kuweka wazi kuwa hana mpango wa kulipiza kisasi licha ya ugomvi uliojitokeza kati yao.

"Mimi ni Mkristo. Mimi sitakuwa na maneno na wewe. Nitahakikisha kuwa umeenda nyumbani polepole na upumzike uendelee na maisha yako uniachie Kenya hii niiskume mbele," Alisema.

"Wachana na William Ruto. Nilikuunga mkono wakati ulinihitaji. Kama hutaki kuniunga mkono niache! Tafadhali!" DP alimwambia Uhuru.

Pia alisisitiza kuwa alimsaidia rais Kenyatta  kupata uongozi na kumtaka kuonyesha shukran kwa usaidizi wake.

"Hufai kuwa chanzo cha vitisho Kenya. Wacha kutisha Wakenya. Kazi yako ni kuhakikisha Wakenya wako salama. Wacha kutuambia ati tutakujua wewe ndiye rais. Sisi ndio tulikuchagu uwe rais wa Kenya. Wacha kututisha. Sisi sio watu wa kutishwa," Alisema.

Naibu rais alidokeza ugomvi zaidi wa ndani  kati yake na rais Kenyatta huku akimuomba asidhuru watoto wake.

"Rafiki yangu bwana rais, tafadhali kuwa muungwana. Kuwa na shukrani, sisi ndio tulikusaidia.  Tafadhali.. Wacha kujifanya saa hizi sijui unajifanya nini. Eti sasa wewe unaanza kunitishia mimi! Eti utanifanya nini.. bora usidhuru watoto wangu. Lakini mimi na wewe tuheshimiane tafadhali," Ruto alisema.

View Comments