In Summary

•Katika taarifa yake ya Jumanne, Gidi alifichua kwamba  alikuwa anaugua kwa muda siku kadhaa zilizopita.

•Takriban wiki tatu zilizopita, Gidi alifichua kwamba alikuwa amelazwa hospitalini baada ya kuugua.

Mtangazaji Gidi Ogidi

Mtangazaji mashuhuri wa kipindi pendwa cha Gidi na Ghost Asubuhi kwenye Radio Jambo, Joseph Ogidi almaarufu Gidi Gidi amekiri kwamba amepungua uzito kiasi wa mwili katika siku za hivi majuzi.

Katika taarifa yake ya siku ya Jumanne, Gidi alifichua kwamba  alikuwa anaugua kwa muda siku kadhaa zilizopita.

Mtangazaji huyo mahiri hata hivyo aliweka wazi kwamba kwa bahati nzuri, kwa sasa amepata nafuu kikamilifu.

"Habari za asubuhi, ndio nimepoteza kilo kadhaa, nilikuwa mgonjwa lakini sasa nimepata nafuu," alisema kupitia Instagram.

Kufuatia hilo, Gidi alitoa shukrani za dhati kwa Maulana kwa kumwezesha kurejesha afya nzuri baada ya kuugua.

Alidokeza kuwa aliugua baada ya kula chakula kilichoharibika na hivyo kuwaonya watu kuwa waangalifu na kile wanachokula.

"Jihadharini na muangalie kile mnachokula, kuharibika kwa chakula ni kweli," alisema.

Takriban wiki tatu zilizopita, Gidi alifichua kwamba alikuwa amelazwa hospitalini baada ya kuugua.

Kwenye ukurasa wake wa Instagram, mtangazaji huyo alichapisha picha yake akiwa katika chumba cha wagonjwa huku akiwa na sindano kwenye mkono wa kushoto na akabainisha kuwa anapata nafuu.

"Siku ya tatu ya sindano ya IV, nahisi vizuri zaidi," alisema kwenye ukurasa wake wa mtandao wa Instagram.

Kwa siku mbili, mashabiki wa kipindi maarufu cha Gidi na Ghost Asubuhi Radio Jambo asubuhi walikosa sauti ya Gidi huku mtangazaji mwenzake Ghost Mulee akiendesha kipindi hicho peke yake.

Wakati huo, Ghost alifichua kuwa mwenzake alikuwa amechukua mapumziko mafupi na akadokeza kuwa angerejea baada ya siku chache.

"Leo hatupo na bosi wangu. Kesho (Ijumaa) pia hatutakuwa naye. Bosi wangu amechukua mapumziko kidogo. Natumai tutakuwa naye Jumatatu," Ghost alisema wakati wa kipindi cha asubuhi.

Mashabiki wa Gidi walimtakia afueni ya haraka kwenye redio na kupitia kurasa zake za mitandao ya kijamii.

View Comments