In Summary

•Akothee alizungumza kuhusu mipango ya harusi kubwa sana hivi karibuni ambapo atafunga ndoa rasmi na mpenzi wake Nelly Oaks.

•“Kuna wachawi wengi.. Wakati huu hatutangazi tarehe, itakuwa ya mwaliko. Na mwaliko utakuwa kulingana na utajiri wako,” alisema.

Image: HISANI

Msanii na mjasiriamali maarufu wa Kenya Esther Akoth almaarufu Akoth alikuwa mgeni wetu katika kipindi cha Gidi na Ghost Asubuhi siku ya Jumanne asubuhi.

Msanii huyo mwenye umri wa miaka 43 alizungumza kuhusu masuala mbalimbali ikiwa ni pamoja na masuala ya kibinafsi, biashara na nafasi yake ya ubalozi wa utalii wa Uganda.

Pia alizungumza kuhusu mipango ya harusi kubwa sana hivi karibuni ambapo atafunga ndoa rasmi na mpenzi wake wa sasa Nelson Oyugi almaarufu Nelly Oaks.

“Ile harusi nyingine (na Omosh) ni ndogo, ile ilikuwa ni mazoezi tu. Harusi inakuja saa hii. Kuna ingine kubwa,” Akothee alisema.

Aliweka wazi kuwa licha ya changamoto ambazo amekumbana nazo katika mahusiano na ndoa zake za awali, bado hajapoteza matumaini katika mapenzi.

“Kwa nini nipoteze matumaini na mapenzi? Nahitaji kupendwa. Nitaenda kufanya harusi nyingine. Hii sasa itakuwa ya kimataifa. Mshikaji anajulikana,” alisema.

Mama huyo wa watoto watano hata hivyo alikataa kufichua maelezo mengi kuhusu harusi yake ijayo, akibainisha kuwa kuna watu wengi ambao hawawatakii wengine mema.

Hata hivyo alisema kuwa wageni wataalikwa kulingana na thamani yao.

“Kuna wachawi wengi.. Wakati huu hatutangazi tarehe, itakuwa ya mwaliko. Na mwaliko utakuwa kulingana na utajiri wako,” alisema.

Akothee na Nelly Oaks wamekuwa wakisherehekea mapenzi yao waziwazi katika miezi kadhaa iliyopita, baada ya kurudiana tena kufuatia kuvunjika kwa ndoa ya Akothee na ex wake Denis Schweizer katikati mwa mwaka uliopita.

Mwishoni mwa mwaka jana, mwanamuziki huyo  alionekana kuthibitisha kufufuka kwa mahusiano yake na Nelly Oaks katika kipindi cha moja kwa moja kwenye mtandao wa TikTok.

Katika kipindi hicho, Akothee alisikika akimwita meneja huyo wake ‘babe’ mara kadhaa, jina ambalo hutumika sana sana  wapenzi.

Nelly Oaks pia alisikika akimtaja Akothee kama mtu maalum kwake huku wawili hao wakishiriki matukio ya kimapenzi kwenye kamera.

“Hiki ni chakula cha jioni maalum kwa mtu maalum kama wewe. Ni surprise,” Nelly Oaks alisikika akimwambia mwanamuziki huyo.

Wakati baadhi ya mashabiki walipotaka kujua iwapo Nelly Oaks ana mchumba, mwanamuziki huyo mwenye umri wa miaka 43 alionekana kuthibitisha kuwa yeye ndiye anashikilia nafasi hiyo.

“Ati kama Nelly ako na mtu?! Kwani mimi mawe? Mimi mawe? Ama mimi ni mti? Unauliza kama Nelly ako na mtu, kwani mimi ni mawe? Ama kijiti? Usinipimie pumzi. Maisha ni ya kwangu nayaendesha vile nataka,” alisema.

Nelly Oaks pia aliweka wazi kuwa hapatikani kwa mwanamke mwingine.

Hapo awali mwanamuziki huyo amewahi kuolewa rasmi mara mbili, ya kwanza na mume wake wa kwanza Jared Okello na ya pili na mzungu Denis Schweizer almaarufu Mister Omosh.

View Comments