In Summary

•Melody alisema kwamba amepata msukumo wa muziki kutoka kwa wasanii kadhaa wa Bongo wakiwemo Ali Kiba na Diamond.

•Nchini Kenya, Melody alisema anawapenda wasanii wengi ambao ameweza kuzoa msukumo mkubwa kwao.

Image: INSTAGTAM// JAY MELODY

Staa wa Bongo Sharif Said Juma almaarufu Jay Melody ameweka wazi kwamba anawatambua wasanii wenzake wengi wa Tanzania.

Akiwa katika mahojiano na Massawe Japanni kwenye Bustani la Massawe kituoni Radio Jambo, Melody alisema kwamba amepata msukumo wa muziki kutoka kwa wasanii kadhaa wa Bongo wakiwemo Ali Kiba na Diamond.

"Napenda wasanii wengi sana. Namtambua Ali Kiba, Lady Jay Dee nyimbo zake ni nzuri, Diamond.." alisema.

Mwanamuziki huyo mwenye umri wa miaka 25 alikubali kuwa Diamond ameendelea kutesa licha ya kuwa kwenye tasnia ya Bongofleva kwa muda mrefu.

Pia alibainisha kuwa nyimbo za Lady Jaydee bado zinaendelea kushabikiwa na wengi licha ya kuwa uimbaji wake umefifia sana kwa sasa.

Nchini Kenya, Melody alisema anawapenda wasanii wengi ambao ameweza kuzoa msukumo mkubwa kwao.

"Nawapenda watu wengi Kenya. Napata msukumo kwa wasanii wa Kenya. Nawapenda kina Otile Brown, Jovial Mejja, Masauti," alisema.

Alisema kuwa nyimbo za Kenya zinachezwa na kupendwa sana nchini Tanzania hasa jijini Dar es Salaam.

Wakati wa mahojiano hayo, mwanamuziki huyo kijana pia alifunguka kuhusu safari yake ya muziki kuanzia akiwa mwandishi wa nyimbo hadi kuimba nyimbo zake.

Melody aliweka wazi kwamba taaluma yake ya muziki ilingo'a nanga vizuri takriban miaka sita iliyopita baada ya kuwachia kibao 'Goroka'

"2017 nilipata kutoa wimbo 'Goroka' ambao ulinitoa zaidi. Ulitamba sana nchini Tanzania. Mwaka wa 2021 nilitoa 'Huba Hulu' ambao ulipata kuvuma hata hapa Kenya," alisema.

Mwimbaji huyo wa kibao 'Sugar' alikiri kuwa mwanzoni alikabiliwa na changamoto kubwa ya kuwaaminisha watu kuwa anajua kuimba.

"Huwezi kupata favour ya mtu kukupokelea vizuri mwanzoni. Wakati mwingine unaweza kukataliwa kwenye radio," alisema.

Pia alidokeza kuwa alikabiliwa na tatizo la kukataliwa na baadhi ya wasanii wakubwa wakati bado akiwa msanii chipukizi.

"Kuna wasanii wakubwa unajitahidi kufanya kazi nao lakini hawaoni interest. Wakati mwingine unaweza ukaweka vesi yako kwa wimbo kisha ikatolewa kwa sababu bado hujapata kusikika. Lakini sasa siwezi kukataliwa mimi ni msanii mkubwa,"

Melody yuko nchini Kenya kwa ziara ya siku nne na ameratibiwa kutumbuiza mjini Nanyuki na Kisumu.

View Comments