In Summary

•Mtangazaji Gidi Gidi ameelezea kukerwa kwake na tukio hilo na kubainisha kuwa ni zaidi ya uwendawazimu.

•Polisi wanaripoti kwamba mwanamke huyo alimkata mtoto wake vipande vipande kabla ya kula matumbo na figo zake.

Mtangazaji Gidi Ogidi

Mtangazaji wa kipindi cha Gidi na Ghost asubuhi kwenye Radio Jambo, Gidi Ogidi amesikitishwa na kisa cha kuhuzunisha cha mwanamke kutoka eneo la Kitengela ambaye alimuua mtoto wake kwa kisu kisha kula viungo vyake.

Bi Olivia Naseren ,27, anazuiliwa katika kituo kimoja cha polisi cha kaunti ya Kajiado baada ya kukamatwa kwa madai ya kumchoma kisu binti yake wa miaka miwili  zaidi ya mara 100 kisha kula baadhi ya viungo vyake.

Kupitia ukurasa wake wa Facebook, Gidi ameelezea kukerwa kwake na tukio hilo na kubainisha kuwa ni zaidi ya uwendawazimu.

"Najua kuna nyakati za ukichaa wa muda, lakini tukio la mwanamke huyo wa Kitengela ni zaidi ya uwendawazimu," alisema.

Haya yanajiri wakati video ya Olivia Naseren akimdunga kisu bintiye zaidi ya mara mia moja ikiendelea kusambaa kwenye mitandao ya kijamii. Wakenya wameendelea kuelezea ghadhabu yao kutokana na tukio hilo.

Ripoti zinaonyesha kuwa mwanamke huyo alimdunga kisu binti yake baada ya kuachana na mzazi mwenzake.

Polisi wanaripoti kwamba mwanamke huyo alimkata mtoto wake vipande vipande kabla ya kula matumbo na figo zake.

Wakazi wa eneo ambao walitazama masaibu hayo kutoka kwenye madirisha ya nyumba ya mwanamke huyo waliachwa na mshtuko mkubwa wasijue la kufanya. Hawakuweza kumwokoa mtoto huyo kwani mshukiwa alikuwa ameifungia nyumba yake kwa ndani kwa kufuli mbili.

Kabla ya kitendo hicho cha kinyama, inaripotiwa kuwa Naseren alianza kwa kuvunja vyombo vyake vya nyumbani.

Baadaye, maafisa wa polisi waliokuwa wameitwa kwenye eneo la tukio walifanikiwa kuingia katika nyumba yake na kumpata akiwa amepoteza fahamu.

"Mtoto mwenye umri wa miaka miwili alikatwakatwa na mamake vipande vipande, na baadaye alikula matumbo yake. Mshukiwa alipatikana katika eneo la tukio akiwa amepoteza fahamu na kupelekwa katika Hospitali ya Kaunti Ndogo ya Kitengela kwa matibabu," ripoti ya polisi ilisoma.

Alipofikishwa hospitalini, mshukiwa alilazimika kutapika viungo vya mtoto huyo alivyodaiwa kula na sasa zitatumika kama ushahidi. Marehemu bintiye alipelekwa katika chumba cha maiti cha Hospitali ya Kaunti Ndogo ya Kitengela.

View Comments