logo

NOW ON AIR

Listen in Live

Patanisho: Mwanadada akataa ndoa na jamaa aliyemsomesha wiki chache kabla ya harusi

Alieleza kuwa mizozo mbalimbali ilitokea baina yake, mumewe na hata familia kabla ya harusi.

image
na Radio Jambo

Makala06 June 2022 - 05:35

Muhtasari


•Jemimah alisema uamuzi wake ulimvunja moyo Shadrack kwa kuwa tayari alikuwa amejitolea kumuelimisha.

•Jemimah alisema amelazimika kumuomba Shadrack msamaha kwa kuwa hajakuwa na amani na amekuwa akisumbuliwa na hisia ya hatia

Gidi na Ghost

Jemimah alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na aliyekuwa mpenzi wake ambaye walikosana takriban miaka minne iliyopita baada ya harusi yao kugonga ukuta.

Mwanadada huyo  alisema roho yake ilikataa ndoa na Shadrack wiki chache tu kabla ya tarehe ya harusi yao.

Jemimah alisema uamuzi wake ulimvunja moyo Shadrack kwa kuwa tayari alikuwa amejitolea kumuelimisha.

"Alinisomesha na nikakataa anioe. Tulikuwa tumeelewana anipeleke chuo kikuu. Alinipeleka na akalipa karo yote. Ikiwa imebaki wiki kadhaa kabla ya harusi yetu roho yangu ilikataa, nikamvunja moyo," Jemimah alisema.

Alieleza kuwa mizozo mbalimbali ilitokea baina yake, mumewe na hata familia kabla ya harusi, hali ambayo alisema ilichangia kusambaratika kwa mipango ya harusi.

"Tulikuwa tumeanza kugombana kuhusu mambo tofauti. Vitu vingi vilitokea nikaona siwezi kulazimisha," Alisema.

Jemimah alisema amelazimika kumuomba Shadrack msamaha kwa kuwa hajakuwa na amani na amekuwa akisumbuliwa na hisia ya hatia.

Shadrack hata hivyo hakuweza kuzungumza  sana alipopigiwa simu kwa kuwa alikuwa ameshikika darasani akifunza.

"Niko darasani, sitaweza kuongea," Shadrack alisema kabla ya kukata simu.

Jemimah alifichua kuwa mpenzi huyo wake wa zamani aliwahi kujaribu kumtafuta ila akahofia kukutana naye.

"Mwaka wa 2020 nilijaribu kumuomba msamaha akaniambia tukutane, niliogopa kukutana na yeye kwa sababu alikuwa ananitishia," Alisema.

Jemimah ambaye aliweka wazi kuwa bado hajaweza kupata mpenzi mwingine aliomba mumewe akubali msamaha ili aweze kupata amani.


RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved