Katika kitengo cha Patanisho, Josephine (20) kutoka Gachie alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na mume wake Brian (22).
Josephine alisema mambo hayajakuwa mazuri katika ndoa yake ya miaka miwili katika kipindi cha takriban miezi miwili iliyopita.
"Nina ujauzito wa miezi miwili lakini sina amani katika ndoa yangu. Kila wakati makosa ikitokea ananipiga kofi. Hii mambo ilianza mwezi wa nne," Josephine alisimulia.
Aliendelea, "Wiki jana nilikuwa natokwa damu nikamwambia alafu akaniambia ni shida yangu kama nimetoa mimba yake hata nikikufa ni shida yangu. Jioni alipokuja alianza kuleta shida, ikabidi nimepigia mamangu nikamwambia. Mama alituongelesha nikadhani iliisha lakini kwake haikuwa imeisha. Sikuweza kuona daktari, nangoja siku yangu ya kwenda clinic tarehe 18."
Josephine aliomba kusaidiwa kupatana na mumewe huku akisisitiza kwamba anampenda sana na hangependa kumpoteza.
Hata hivyo, Brayo alipopigiwa simu alikata muda mfupi baadaye baada ya Gidi kumtaarifu sababu ya kumtafuta.
Josephine aliendelea kufunguka masaibu anayopitishwa na mumewe ikiwa ni pamoja na jinsi anavyotangamana na wasichana wengine.
"Akipatana tu msichana wanakumbatiana ata tukiwa na yeye. Hug zingine huwa salamu, zingine hee.. Nikimuuliza anasema ni hali inafanya. Nikimuuliza ni hali gani inafanya, hajawahi kunifafanulia. Ananiambia hadi mimi nianze kukumbatiana na wanaume tutoshane. Mtu anakumbatiana zaidi ya dakika moja ni hug tu kweli? Anakumbatiana hadi anakwamilia hapo," alisema Josephine.
Josephine alifichua kwamba Brian bado hajapiga hatua ya kwenda kujitambulisha nyumbani kwao. Pia alifichua kwamba mtoto wao wa kwanza anaishi na mama yake ili kuwapa nafasi ya kutafuta riziki.
"Siishi na babangu. Brian ni yatima. Mtu tu anaweza tatua shida yetu ni mama yangu," alisema.
Je, ungemshauri vipi Josephine?