Benson Mutandi, 38, kutoka kaunti ya Kakamega alipeleka ombi katika stesheni ya Radio Jambo, kitengo cha Patanisho akitaka kupatanishwa na babake mwenye umri wa miaka 63.
Benson alisema walikosana na babake mwezi Juni 2023 baada ya kuchukua pesa Zaidi ya kiasi alichokiomba kutoka kwake baada ya kuuza kipande chake cha ardhi.
“Kuna sehemu alikuwa amenipa, nusu ekari na wakati nilitaka kuuza hiyo sehemu niende ninunue kwingine, wakati niliuza, mzee aliniambia nikampa 30k kwa hiyo pesa ya shamba na wakati niliuza sikupewa pesa yote. Yote nilikuwa nimeuza 300k. Mara ya kwanza nilipewa 200k, nikampa 30k penye alitaka, ikawa ningoje hiyo ilibaki lakini akashindwa na kuuzia mwingine. Nikatafuta mnunuzi mwingine naye tena akanipa pesa kidogo na kubaki na 27k.”
“Nikasikia mzee amewashtaki anataka apewe hiyo pesa na baadae akapewa hiyo pesa yote yenye ilibaki…wakati alichukua hiyo pesa sasa mimi nilikuwa nataka nimuombe msamaha hata kama amechukua …” alisema Benson.
Kijana huyo pia alisema kwamba babake alimkataa na hata hakumsomesha wala kumpa kibali cha kutahiriwa.
“Nilitahiriwa kwa barabara sababu mzee babangu alinikataa.”
Benson alisema aliuza shamba na kutaka kwenda mbali na nyumbani kwa sababu maisha ya nyumbani yalimshinda na hata nyumbani walifukuza wake zake 3 na mke wa sasa ni wa nne, akisema kuwa mzee wake alikataa kumchukua shule.
Mzee alipopigiwa simu, alisema yeye hana shida na mtoto wake akisema kwamba amekubali kumsamehe licha ya kuwa Benson amekuwa akimtukana kuwa ana majini.
Mzee alisema Benson alimfuata mamake na kwenda kulelewa huko lakini akarudi akiwa na miaka 19 kabla ya mzee kumpa shamba.
Baada ya kukorofishana, Mzee alisema kwamba kijana wake alianza kumtukana akisema ni mbaya na kuwa ana majini, lakini hatimaye akakubali kumsamehe na kumtaka kurudi nyumbani.
“Nasema msamaha nimemkubalia akuje nyumbani tu na hata kuna shamba nyingine nataa kumpa aniletee hata wajukuu,” mzee alisema.