Katika kitengo cha Patanisho, Bernard Bosire (42) kutoka kaunti ya Kisii alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na mke wake Lydia Kerubo (32) ambaye alikosana naye hivi majuzi kuhusiana na masuala ya kifedha.
Bosire alisema ndoa yake ya miaka saba ilisambaratika siku tatu zilizopita baada ya mke wake kutoridhika na fedha alizomtumia.
"Yeye ako nyumbani, mimi nafanya kazi Kisii. Juzi alafu nikamtumia pesa ingine hapo, akaona kama ni kidogo. Ndio nilikuwa nimeanza kazi, nikalipwa nusu. Nilimpigia simu mara tatu, akakataa kushika. Baadaye alishika akaanza kuniongelesha vibaya. Nilijaribu kumueleza lakini hatukuelewana," Bosire alisema.
Alisisitiza kwamba kabla ya kuanza kazi yake mpya, alikuwa akiwajibika na kushughulikia majukumu yote ya nyumbani.
Bi Kerubo alipopigiwa simu hata hivyo alimkana mzazi huyo mwenzake na kubainisha kwamba hamjui.
"Huyo simjui. Mimi simjui!" alisema kabla ya kukata simu.
Bosire alipopewa nafasi ya kuzungumza naye hewani, alimwambia, "Mama Jane, mimi nakupenda. Na sitaki tena upotee. Urudi kwa ndoa tukae kwa amani."
Je, ushauri ama maoni yako kuhusu Patanisho ya leo ni yepi?