MWANAWE ALIAGA ALIPOKUWA ANAZALIWA

Mwanamuziki wa Gengetone atafuta haki ya mwanawe aliyeaga katika harakati ya kuzaliwa

Lexy Yung wa kikundi cha sailors analaumu muuguzi katika hospitali ya Limuru kwa kumdunga mwanawe akiwa bado tumboni mwa mpenzi wake

Muhtasari

•Yung amelaumu muuguzi huyo kwa kumpokonya mwanawe ambaye alikuwa amesubiria kwa hamu sana. huku akiapa kuwa ni sharti atafute haki ya mwanawe

•Mpenzi wa Yung, Muthoni almaarufu kama @sexy_wa_lexxy, amesema kuwa amekubali mwanawe kupumzika kwa amani huku akisema kuwa ilikuwa kazi ya Mungu na haiwezi kosolewa.

Lexy Yung na Mpenzi wake Faith Muthoni
Lexy Yung na Mpenzi wake Faith Muthoni
Image: Hisani

Mmoja wa wasanii kwenye  kikundi cha Sailors Gang, Lexy Yung pamoja na mpenzi wake Faith Muthoni wanaomboleza kupoteza kitinda mimba chao wakati alikuwa anazaliwa.

Lexy Yung
Lexy Yung
Image: Instagram

Kupitia ukurasa wa Instagram, yung amesema kuwa wawili hao walikuwa wanatarajia mtoto wao wa kwanza usiku wa Ijumaa baada ya Muthoni kupata uchungu wa uzazi na kulazwa katika hospitali ya Limuru.

Mwanamuziki huyo wa nyimbo aina ya gengetone analaumu hospitali ya Limuru kwa kile alichosema ni utepetevu wa mkunga aliyekuwa anasaidia mpenziwe kuzaa.

"Ni msumari uliodungwa kwenye moyo wangu na wa mke wangu.. Tumekuwa na raha tele na tumejitayarisha kumpokea kitinda mimba wetu. Siku hiyo hatimaye ilifika, Juni 4 na ambapo tulipata uchungu wa uzazi mida ya usikuna tukaenda katika hospitali ya Limuru almaarufu kama Patel. Bibi yangu alilazwa na nikaagizwa niende nyumbani nirudi asubuhi ifuatayo. Siku iliyofuata nilirejea hospitali nikiwa nimejawa na raha tele ila habari za kuhofisha zilikuwa zimenisubiria. Muuguzi alipasua maji ya bibi (sijui kama yafaa kupasuliwa) na katika harakati hiyo akadunga mtoto wangu aliyekuwa mzima" Yung aliandika kwenye ukurasa wake wa Instagram.

Msanii huyo amesema kuwa alielezwa na daktari kuwa mtoto wake alikuwa amedungwa katika harakati ya muuguzi kupasua maji ya mkewe.

Yung amelaumu muuguzi huyo kwa kumpokonya mwanawe ambaye alikuwa amesubiria kwa hamu sana. huku akiapa kuwa ni sharti atafute haki ya mwanawe.

Kwa upande wake Muthoni almaarufu kama @sexy_wa_lexxy amesema kuwa amekubali mwanawe kupumzika kwa amani huku akisema kuwa ilikuwa kazi ya Mungu na haiwezi kosolewa.

"Mungu anapeana na anachukua pia kwani anajua mipango aliyo nayo kwetu . Namuachia kila kitu kwani siwezi beba uchungu huo tena. Nashukuru mpenzi wangu Lexy Yung kwa kuwa nami na kuhisi uchungu wangu pia, wewe ni tuzo la maana sana Mungu alilonipa" Faith aliandika kwenye mtandao wa Instagram.

Yung ameeleza kuwa alikuwa amejipanga kabisa kupokea mtoto huyo akisema kuwa alikuwa ashanunua manguo na vitu zingine ambazo mtoto angehitaji ila hakuweza kumsherehekea mwanawe.