Wapenzi Vera Sidika na Brown Mauzo waadhimisha mwaka mmoja wa ndoa yao kwa mtindo wa kipekee

Siku chache zilizopita Vera alishangaza wanamitandao baada ya kukiri kuwa uhusiano wake wa sasa na mwanamuziki Brown Mauzo ndio mrefu zaidi kuwahi tokea maishani mwake.

Muhtasari

•Wapenzi hao walitumia mtandao wa Instagram kusherehekeana huku kila mmoja wao akiandikia mwenzake ujumbe maalum wa kuadhimisha siku maalum maishani mwao.

•Vera alieleza kipenzi chake kuhusu mapenzi makubwa aliyo nayo kwake na kusema kwamba ni matumaini yake kuwa wataendelea kufurahia maisha pamoja kwa miaka mingi

•Kwa upande wake Mauzo alisema kuwa amefurahia kipindi cha mwaka mmoja ambacho kimetamatika na kumhakikishia Vera kuwa wataendelea vivyo hivyo hadi milele.

Image: INSTAGRAM//VERA SIDIKA

Wazazi watarajiwa Vera Sidika na Brown Mauzo hivi leo (Agosti 12, 2021) wanaadhimisha mwaka mmoja wa kuwa pamoja kwa ndoa.

Wawili hao walijitosa kwenye ndoa mnamo Agosti 12 mwaka uliopita na mapenzi yao yameendelea kunoga huku sasa wakiwa safarini kuanzisha familia ndogo.

Wapenzi hao walitumia mtandao wa Instagram kusherehekeana huku kila mmoja wao akiandikia mwenzake ujumbe maalum wa kuadhimisha siku maalum maishani mwao.

Kwenye ukurasa wake, mwanasoshalaiti Vera alipakia video na picha zilizoonyesha baadhi ya kumbukumbu maalum katika safari yao ya ndoa kufikia sasa.

Vera alieleza kipenzi chake kuhusu mapenzi makubwa aliyo nayo kwake na kusema kwamba ni matumaini yake kuwa wataendelea kufurahia maisha pamoja kwa miaka mingi.

"Maadhimisho ya mwaka mmoja yenye furaha kwa mtu pekee duniani ambaye nataka kuwa kando yake kila mchana na usiku maishani mwangu. Nakupenda sana mpenzi.  Na tupate miaka mingi ya furaha pamoja" Vera aliandika.

Kwa upande wake Mauzo alisema kuwa amefurahia kipindi cha mwaka mmoja ambacho kimetamatika na kumhakikishia Vera kuwa wataendelea vivyo hivyo hadi milele.

"Siku 365 za kuwa pamoja kama gundi. nyakati nyingi za furaha, wiki 52 za furaha, kumbukumbu nyingi, dakika 525,600 zimepita na tunaendelea kuhesabu... mazuri bado hayajakuja, maadhisho ya mwaka mmoja yenye fanaka mke wangu. Mwaka mmoja umeisha, hadi milele" Mauzo aliandika.

Siku chache zilizopita mwanasoshalaiti huyo wa miaka 31 alishangaza wanamitandao baada ya kukiri kuwa uhusiano wake wa sasa na mwanamuziki Brown Mauzo ndio mrefu zaidi kuwahi tokea maishani mwake. 

Vera Sidika alifichua kuwa kamwe hajawahi kuchumbia mwanaume mmoja kwa kipindi cha zaidi ya mwaka mmoja hapo awali.

Alipoulizwa na shabiki mmoja kuhusu uhusiano wake na kipenzi cha moyo wake cha sasa alisema kuwa alifurahia kila hatua.

"Imekuwa baraka. Ndio uhusiano mrefu zaidi. Mwaka mmoja sasa" Vera alisema

Vera anatarajia kujifungua mtoto wa kike ifikapo mwezi Novemba mwaka huu.