'Walikung'uta yote!' Mchekeshaji Smart Joker asimulia alivyoibiwa na 'slay queens' waliokuwa wamejihami kwa bunduki

Smart Joker alikiri kuwa pesa zilizosalia baada ya kumnunulia mama yake shamba maeneo ya Lugari kaunti ya Kakamega zilimalizwa na wanadada wanaofahamika kama 'slay queens'.

Muhtasari

•Smart Joker alisema kuwa alitumia kiasi fulani cha pesa alizolipwa na idara ya mawasiliano nchini (CAK) kwa kufanya tangazo la uhamiaji wa kutoka mitambo ya kale hadi ya kisasa mwaka wa 2014 kununulia mama yake shamba.

•Mchekeshaji huyo alisimulia kisa kimoja ambapo 'slayqueens' ambao walikuwa wamejihami na bunduki walimuibia pesa na mali kutoka kwa nyumba aliyokuwa anaishi maeneo ya Kinoo.

Image: FACEBOOK// SMART JOKER

Mchekeshaji Michael Omuka almaarufu kama Smart Joker amesimulia alivyoibiwa kiwango kikubwa cha pesa na mali na wanadada aliokuwa amealika kwa nyumba yake.

Akiwa kwenye mahojiano na Daniel Ndambuki katika kipindi cha Churchill Show, Smart Joker alisema kuwa alitumia kiwango fulani cha pesa alizolipwa na idara ya mawasiliano nchini (CAK) kwa kufanya tangazo la uhamiaji wa kutoka mitambo ya kale hadi ya kisasa mwaka wa 2014 kununulia mama yake shamba.

Smart Joker alikiri kuwa pesa zilizosalia baada ya kumnunulia mama yake shamba maeneo ya Lugari kaunti ya Kakamega zilimalizwa na wanadada wanaofahamika kama 'slay queens'.

"Maslayqueen walikung'uta pesa yote. Kabla nipate Mercy nipate naye watoto wazuri maslayqueen walinichanganya" Smart Joker alisimulia.

Mchekeshaji huyo alisimulia kisa kimoja ambapo 'slayqueens' ambao walikuwa wamejihami na bunduki walimuibia pesa na mali kutoka kwa nyumba aliyokuwa anaishi maeneo ya Kinoo.

"Kwanza hapo Kinoo, wacha tu! Walikuja wakazichukua kwa nyumba.. Imagine umewekewa bunduki mmoja wao anaambia wengine, 'si huyu ni Smart wa Churchill Show' wanasema nitoe pesa. Alafu wameshika kifunguo ya gari wananiuliza kama ni yangu wanachukua.. na saa hiyo mko ndethe kwa kitanda" Smart Joker alisimulia.

Alisema kuwa alikuwa anahifadhi pesa zingine kwa nyumba ili apate za kujiburudisha  na wanawake kwa nyumba.

Hata hivyo mchekeshaji huyo alisema kuwa hatua yake ya kuoa ilimsaidia sana kuepuka masaibu kama yale.

Msanii huyo ni balozi rasmi wa idara ya mawasiliano nchini (CAK).