"Fagia wote!" Mchekeshaji Eric Omondi apendekeza bwenyenye Jimi Wanjigi kuwa rais wa Kenya

Muhtasari

• Eric amesema kuwa wakati umewadia kwa wale wote ambao wamekuwa uongozini kwa miaka mingi kuenda nyumbani na kuachia viongozi wapya usukani.

Image: INSTAGRAM

Mchekeshaji Eric Omondi amependekeza bilionea Jimi Wanjigi kuwa rais wa Kenya mwaka baada ya kustaafu kwa Uhuru Kenyatta mwaka ujao.

Kupitia kampeni iliyobandikwa jina 'Fagia wote', Eric amesema kuwa wakati umewadia kwa wale wote ambao wamekuwa uongozini kwa miaka mingi kuenda nyumbani na kuachia viongozi wapya usukani.

"Hatutaki majina zinajulikana. 2022 tunawafagia wote. Vijana tumeamka na tunakuja" Omondi alisema kwenye video aliyopakia kwenye ukurasa wake wa Instagram.

Omondi amesema kuwa kinara wa ODM Raila Odinga, naibu rais William Ruto, kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka na mwenzao wa ANC Musalia Mudavadi wameshindwa kusukuma nchi mbele na kuwataka wasiwanie viti hivyo mwaka ujao.

Mchekeshaji huyo amewasihi vijana kutopigia kura viongozi ambao wamekuwa serikalini hapo awali na badala yake wachague viongozi wapya.

Amelalamikia shida mbali mbali ambazo zimekosa kushughulikiwa kwa miaka mingi haswa kwenye sekta ya elimu na ajira.

"Walitwambia eti tutapata kazi tukiwachagua lakini kwa hii nchi mahali kuna Job ni kwa Bibilia peke yake.. Raila, Kalonzo, Ruto, Mudavadi wakati wenu umefika na msipotusikia mnaenda nyumbani. 2022 wazee wote mnaenda nyumbani" Alisema Omondi.

Kulingana na Omondi , Wanjigi ndiye bora kuchukua usukani kwani yeye ni mgeni  serikalini na anaelewa biashara.

Mfanyibiashara ashatangaza azimio lake kuwania kiti cha urais mwaka ujao kwa tikiti ya ODM. Anatazamia kumbandua Raila Odinga kwenye kura za uteuzi wa mpeperusha bendera wa chama hicho.