Juliani apiga ripoti baada ya kutishiwa maisha yake kwa kuchumbia aliyekuwa mke wa gavana Mutua

Muhtasari

•Mwanamuziki huyo alionywa dhidi ya kupakia picha alizopiga pamoja na Lilian kwenye mitandao ya kijamii na kutishiwa kuuawa iwapo angeendelea

Image: INSTAGRAM

Mwanamuziki Julius Owino almaarufu kama Juliani amepiga ripoti kuhusu vitisho dhidi ya maisha yake alivyopokea baada ya kuvunja kimya kuhusu uhusiano wake na Bi. Lilian Ng'ang'a.

Siku ya Jumatano mida ya jioni mwanamuziki huyo alifichua kuwa alikuwa amepigiwa simu na kutumiwa jumbe za vitisho punde baada ya kuzungumzia uhusiano wake na aliyekuwa mke wa gavana wa Machakos Alfred Mutua.

Mwanamuziki huyo alisema kuwa simulizi ya kunyang'anyana mke ni jambo la uongo na kusema kuwa hakuna vile mtu mzima anaweza 'kuibiwa'

"Unawezaje 'kuiba' mtu? Mtu mzima mwenye akili timamu! "Simu niliyopigiwa na ujumbe wa vitisho dhidi ya maisha yangu ambao nilipata leo sio jambo la kufurahisha! Simulizi ya 'Ulinyang'anyana ni ya uongo, ya kuchokesha na vichwa  tamu vya habari tu. Tafadhali wacheni" Juliani aliandika kwenye ukurasa wake wa Twitter.

Kwenye ujumbe wake msanii huyo alimuagiza aliyekuwa anampa vitisho iwapo ataamua kuvitekeleza asiharibu sura yake kwani angependa kuzikwa akiwa anatabasamu.

"Kwa vitisho, usipime uso, ningependa kutabasamu ndani ya kaburi langu" Juliani alisema.

Mwanamuziki huyo alionywa dhidi ya kupakia picha alizopiga pamoja na Lilian kwenye mitandao ya kijamii na kutishiwa kuuawa iwapo angeendelea.

Adhuhuri ya Alhamisi Juliani  aliamka na kufululiza moja kwa moja hadi kituo cha polisi cha Kileleshwa ambapo alipiga ripoti na kuandikisha taarifa kuhusu vitisho hivyo.