"Mkeo sio mtumwa" Boniface Mwangi akemea wanaume wanaoamsha wake zao usiku kuwapikia, awaita wadhaifu na wasiojithamini

Muhtasari

• Mwanaharakati huyo amesema kuwa wanaume wenye tabia ya kuamsha wapenzi wao usiku wapike wanapofika nyumbani wakiwa wamechelewa ni wadhaifu na hawajidhamini.

Image: INSTAGRAM// BONIFACE MWANGI

Mwanaharakati mashuhuri nchini Boniface Mwangi amewasuta vikali wanaume ambao hufika kwa nyumba usiku wakiwa wamechelewa na kuwaamsha wake zao wawapikie ama wapashe chakula chao motoni.

Kupitia ukurasa wake wa Instagram, mtetezi huyo wa haki za kibinadamu amesema kuwa wanaume wenye tabia kama ile ni wadhaifu na hawajidhamini.

Mwangi amesema kuwa yeye anapofika nyumbani akiwa amechelewa huwa anaelekea jikoni mwenyewe na kujipashia chakula chake motoni bila kumsumbua mkewe.

"Unajua kuna wanaume ambao huwaamsha mabibi wao ili wawapikie ama wawapashie chakula motoni. Hao ni wanaume dhaifu ambao hawajidhamini. Ikiwa wataka mke wako aamke akupashie chakula motoni  basi nenda ukatafute chakula chako, ukitayarishe na uweke mezani. Lakini ikiwa hutafuti chakula chako unanunua dukani basi nenda jikoni ujipashie chakula  motoni mwenyewe.

Naskia kuna wanaume ambao hufika nyumbani wakiwa wamechelewa na kuamsha wake zao ili wawapashie chakula motoni. Mimi ninapofika kwa nyumba nikiwa nimechelewa huwa napasha chakula changu motoni mwenyewe. Mkeo sio microwave. Pasha chakula chako mwenyewe" Mwangi amesema.

Kulingana na Mwangi, mkeo ama mpenzi wako sio mtumwa na hufai kumuamsha unapofika nyumbani usiku ukiwa umechelewa.