Willy Paul atishia kushtaki msanii wa kike aliyedai kuwa alimnyanyasa kingono, amwagiza aombe msamaha

Muhtasari

•Kulingana na Willy Paul, Miss P  anampenda sana  na alitoa matamshi yale kutokana na hasira baada ya kugundua kuwa hawezi kupokea mapenzi kama yale anayo kutoka kwake.

•Wakili wa Willy Paul amesema kuwa matamshi ya Miss P yamemsababishia mwanamuziki huyo chuki, aibu, hasara, dharau, uchungu na madhara mengine mengi.

Willy Paul na Miss P
Image: Hisani

Mwanamuziki Mashuhuri Wilson Ouma Opondo almaarufu kama Willy Paul amemwandikia mwanamuziki Elvira Wambui Maina almaarufu kama Miss P akimtaka kuomba msamaha kufuatia madai aliyotoa kwamba alimlazimisha kushiriki mapenzi bila kinga mara kadhaa wakati walikuwa wanafanya kazi pamoja.

Kupitia ujumbe wa kuchapishwa ambao alipakia hadharani kwenye kurasa zake za mitandao ya kijamii siku ya Jumapili, Willy Paul amesema kuwa madai ya Miss P ni ya uongo, ya chuki na yenye nia ya kumharibia jina tu.

Kulingana na Willy Paul, Miss P  anampenda sana  na alitoa matamshi yale kutokana na hasira baada ya kugundua kuwa hawezi kupokea mapenzi kama yale anayo kutoka kwake Willy.

"Nimeona na kuskia yale yote ambayo yamekuwa yakiendelea kwa siku kadhaa kwenye mitandao ya kijamii kuhusiana na mwanamke anayedai kuwa nilimnyanyasa kingono.Ningependa kila mtu afahamu kuwa hayo ni madai ya kutengenezwa.

Huyo ni mwanamke ambaye ananipenda sana na anafanya yale kutokana na hassira, tulikuwa na wakati wetu ila akagundua  kuwa siwezi kumpa mapenzi kama anayonipa kwa hivyo akatengeneza hadithi ambayo imeniharibia jina" Willy Paul aliandika kwenye ukurasa wake wa Instagram.

Ujumbe huo uliambatana na picha za ujumbe ambao mawakili wake waliandikia Miss P wakimwagiza kusita kueneza maneno ya uongo dhidi ya Willy Paul  na kuomba msamaha la sivyo hatua za kisheria zitachukulia.

Willy Paul ametishia kupeleka kesi ile kortini iwapo Miss P hatafanya kama alivyoagizwa kwenye ujumbe huo.

"Ujue kuwa tusiposkia kutoka kwako kama ulivyoagizwa, tumeelekezwa kuanza kesi dhidi yako kwa madhara uliyosababisha bila kukujulisha. Tunatumai utafuata hayo kuzuia hatua zaidi" Ujumbe wa wakili wa Willy Paul ulisoma.

Kwenye ujumbe huo, wakili wa Willy Paul amesema kuwa matamshi ya Miss P yamemsababishia mwanamuziki huyo chuki, aibu, hasara, dharau, uchungu na madhara mengine mengi. Amesema kuwa hadhi ya Willy Paul kwenye sanaa huenda ikashuka iwapo mwanadada yule ataendelea kueneza chuki dhidi yake.