Mwigizaji mashuhuri wa filamu 'The Wire' apatikana amefariki ndani ya nyumba yake

Muhtasari

•Inatuhumiwa kuwa mwigizaji huyo aliangamia kutokana na utumiaji wa madawa ya kulevya kupita kiasi, ingawa madai hayo hayajathibitishwa bado.

Image: GETTY IMAGES

Mwigizaji wa Marekani Michael K Williams  anayefahamika sana kutokana na filamu 'The Wire' ameaga dunia.

Williams 54, ambaye alicheza kama 'Omar Little' kwenye filamu ya 'The Wire' alipatikana akiwa ameaga ndani ya nyumba yake jijini New York siku ya Jumatatu . Aliigiza kama shoga, jambazi na muuzaji wa madawa ya kulevya.

Inatuhumiwa kuwa mwigizaji huyo aliangamia kutokana na utumiaji wa madawa ya kulevya kupita kiasi, ingawa madai hayo hayajathibitishwa bado.

Mwili wa Williams ulipatikana katika chumba chake cha maakuli huku kichwa chake kikiwa kimetazama chini. Inaripotiwa kuwa poda iliyoonekana kuwa heroin ilipatikana juu ya meza yake.

Baadhi ya waiigizaji wenzake na watengeneza filamu wametuma risala za rambirambi.

Hapo awali, Williams ambaye alikuwa ameteuliwa mara tatu kupokea tuzo la Emmy alikuwa amefunguka kuhusu shida yake ya utumizi wa madawa ya kulevya kwa miaka mingi.