"Ujauzito sio tiketi ya ndoa" Vera Sidika awaonya wanadada wanaotumia mtoto kulazimisha uhusiano na mwanaume

Amewaonya wanawake ambao wanajaribu kuwafunga wanaume kwa kupata watoto nao wakitumai kuwa watafunga ndoa nao

Muhtasari

•Kulingana na Vera, hakuna kitu ambacho kinaweza kumfanya mwanaume ajitose kwenye mahusiano na mwanamke ambaye hataki

•Mama huyo mtarajiwa amewaarifu wanawake kuwa hatua ya kupata mtoto na mwanaume haimaanishi kuwa  watakuwa pamoja milele.

Image: INSTAGRAM// VERA SIDIKA

Mwanasoshalaiti na mfanyibiashara maarufu Vera Sidika amewaonya wanawake dhidi ya kulazimisha mapenzi na wanaume ambao hawawataki.

Kupitia mtandao wa Instagram, Vera amewaagiza wanawake kukubali hatima yao wanapokataliwa na kusonga mbele na maisha yao bila kulazimisha mapenzi.

Kulingana na msanii huyo mwenye umri wa miaka 31, hakuna kitu ambacho kinaweza kumfanya mwanaume ajitose kwenye mahusiano na mwanamke ambaye hataki. Amesema kuwa kupika, kuosha, uaminifu, unyenyekevu, mtoto au mitindo tofauti  ya ngono haziwezi kumfanya mwanaume abadili hisia zake kwa mwanamake.

"Sijui nani anahitaji kuskia haya lakini iwapo mwanaume hakutaki, kweli hakutaki. Hakuna kiwango chochote cha ngono, mitindo ya ngono, kupika, kuosha, uaminifu, kumfunga na mtoto, unyenyekevu  n.k ambazo zitafanya akutake ama ukae. Kubali tu hatima na usonge mbele na maisha.

Kila kitu kingine chawezekana lakini huwezi kulazimisha uhusiano na mtu ambaye hataki kuwa kwenye uhusiano na wewe ama hakutaki tena. Inauma najua  lakini huo ndio ukweli" Vera aliandika kwenye ukurasa wake wa Instagram.

Mama huyo mtarajiwa amewaarifu wanawake kuwa hatua ya kupata mtoto na mwanaume haimaanishi kuwa  watakuwa pamoja milele.

Vera amesema kuwa mtoto sio tikiti ya ndoa au uhusiano wa milele na kudai kuwa mtoto sio sababu tosha ya kufanya mwanaume akae maishani ya mwanamke.

"Kupata watoto na mtu haimaanishi kuwa lazima muwe pamoja milele. Mimba sio tikiti ya uhusiano wa milele au ndoa. Inauma lakini huu ndio ukweli. Ujauzito sio sababu mwenzako atakaa kwenye uhusiano, mpenzi wako atakaa kwa sababu tu anataka kukaa" Vera amesema.

Amewaonya wanawake ambao wanajaribu kuwafunga wanaume kwa kupata watoto nao  wakitumai kuwa watafunga ndoa nao.

"Wanawake wengi wanajaribu kuwatega wanaume na watoto na wanajipata na watoto watano wa baba tofauti. Kwa kutega namaanisha hamkuzungumzia suala la kupata watoto ama kuwa pamoja. Hamkupangia ujauzito. Kuna uwezekano hata kuwa ni mahusiano mapya halafu boom mwanamke anapata ujauzito akitaka huku akidhani kuwa mwanaume atakaa kwenye uhusiano milele. Usijaribu mchezo huu kwa sababu matarajio huishia kwa kuvunjwa moyo" Aliandika Vera.

Mwanasoshalaiti huyo anatarajia mtoto wake wa kwanza hivi karibuni na mpenzi wake Brown Mauzo ambaye wamekuwa kwenye ndoa kwa mwaka mmoja.