"Mungu nifariji, nipe nguvu" Mwanamuziki Size 8 amkumbuka marehemu mamake kwa ujumbe wa kihisia

Muhtasari

•Bi Esther Njeri Munyali aliangamia kutokana na matatizo ya figo mnamo mwezi Novemba mwaka wa 2015, masaa machache tu baada ya Size 8 kujifungua mtoto wake wa kwanza , Ladasha Belle.

Image: INSTAGRAM// SIZE 8

Mwanamuziki mashuhuri Linet Masiro Munyali alimaarufu kama Size 8 amemkumbuka marehemu mamake ambaye aliaga takriban miaka sita iliyopita.

Bi Esther Njeri Munyali aliangamia kutokana na matatizo ya figo mnamo mwezi Novemba mwaka wa 2015, masaa machache tu baada ya Size 8 kujifungua mtoto wake wa kwanza , Ladasha Belle.

Miaka sita baadae mwanamuziki huyo bado hajaweza kukabiliana na majonzi ya kupoteza mamaye mpendwa na kupitia ukurasa wake wa Instagram amemwomba Mola kumpa nguvu na faraja anapoendelea kuomboleza.

"Wakati ambapo mwanamke aliyekomaa anampeza sana mama yake waaah.. Mungu wa faraja yote naomba nifariji, nipe nguvu na neema yako inilinde na nguvu za kuendelea na safari hii kwani kwa nguvu zako naweza kuponda jeshi, nikiwa nawe naweza kupanda ukuta wowote" Size 8 aliandika.

Size 8 hakupata nafasi ya kumzika mama yake wakati aliaga kwani bado alikuwa amelazwa hospitalini akiwa anaugua sana.

Mamake Size 8  alizikwa katika mji wa Mbale nchini Uganda alikozaliwa bwanake.