(Video) Mchekeshaji Mulamwah atunuku mpenzi wake shilingi 100,000 kama zawadi ya kujifungua

Wapenzi hao wawili walikaribisha binti yao duniani siku ya Jumapili.

Muhtasari

•Mulamwah alikuwa ameenda hospitani kumuona mpenzi wake pamoja na bintiye wakati alitunuku zawadi ya pesa na maua.

•Mchekeshaji huyo alieleza raha kubwa  aliyokuwa nayo moyoni mwake baada ya kubarikiwa na mtoto wake wa kwanza  na kudai kwamba siku itimiapo ataonyesha urembo wa bintiye hadharani.

•Mapema mwaka uliopita ndoto ya wawili hao ya kufanya familia yao iwe kubwa ilikuwa imefifia baada ya ujauzito ambao Bi Carol alikuwa amebeba kuharibika.

Image: INSTAGRAM// MULAMWAH

Mchekeshaji David Oyando almaarufu kama Mulamwah amemtunuku mpenzi wake Caroline Muthoni shilingi laki moja baada yake kujifungua mtoto wao wa kwanza.

Wapenzi hao wawili walikaribisha binti yao duniani siku ya Jumapili.

Kwenye video ambayo alipakia kwenye ukurasa wake wa Instagram, Mulamwah alionekana akimwangushia mpenzi wake noti za pesa ambazo zinaaminika kuwa shilingi laki moja.

Mulamwah alikuwa ameenda hospitani kumuona mpenzi wake pamoja na bintiye wakati alitunuku zawadi ya pesa na maua.

"Nimekuletea shilingi laki moja. Ni yako ya kutumia. Fanya  nazo chochote ambacho unataka. Hongera sana kwa zawadi hii nzuri umetuletea. Tunatumai mema kila wakati. Nakupenda sana" Mulamwah alimwambia mpenzi wake alipokuwa anampatia pesa zile. 

Wawili hao walitangaza kuzaliwa kwa binti yao ambaye wamempatia jina Keilah Oyando kupitia kurasa zao za mitandao ya kijamii asubuhi ya Jumatatu.

"Na ni msichana. Muujiza umewasili.. maneno hayaweza kueleza ninavyohisi, ni kitu cha maana zaidi kuwahi fanyika maishani mwangu. Karibu kipenzi @keilah_oyando" Mulamwah aliandika kwenye ukurasa wake wa Instagram.

Msanii huyo ambaye pia ni muuguzi alichukua  nafasi ile kumshukuru mpenzi wake na kumbubujikia sifa kufuatia hatua hiyo.

"Asante mpenzi @carrol_sonie kwa zawadi nzuri. Wewe ni mwanamke jasiri kuweza kufanya haya licha ya yale yote tumepitia. Asante sana kwa waliotutakia mema na kutuombea. Asanteni sana" Mulamwah alisema.

Mchekeshaji huyo alieleza raha kubwa  aliyokuwa nayo moyoni mwake baada ya kubarikiwa na mtoto wake wa kwanza  na kudai kwamba siku itimiapo ataonyesha urembo wa bintiye hadharani.

"Ni mrembo, siwezi subiri kuonyesha walimwengu siku moja na niwe na mazungumzo ya baba na binti. Mimi ni baba mwenye raha. Shukran kwa Mungu" Alisema Mulamwah.

Bi Caroline kwa upande wake aliapa kumpatia bintiye malezi bora zaidi.

"Staa amezaliwa.. nakaribisha kito cha thamani zaidi kwa familia yetu @keilah_oyando. Siwezi subiri kukupa malezi bora" Carol aliandika.

Mapema mwaka uliopita ndoto ya wawili hao ya kufanya familia yao iwe kubwa ilikuwa imefifia baada ya ujauzito ambao Bi Carol alikuwa amebeba kuharibika.