Baadhi ya wasanii mashuhuri ambao wamefungulia watoto wao kurasa za mitandao ya kijamii

Muhtasari

•Baada ya mchekeshaji Mulamwah kukaribisha mtoto wake wa kwanza siku ya Jumatatu, alichukua hatua ya kufungulia bintiye akaunti ya Facebook na ya  Instagram ( @keilah_oyando) ambazo tayari zimepata wafuasi 19,000 na 7,500 mtawalia siku moja tu baadae.

Image: INSTAGRAM

Siku ya Jumatatu mchekeshaji  David Oyando almaarufu kama Mulamwah pamoja na mpenzi wake Caroline Muthoni walitangaza kuzaliwa kwa mtoto wao wa kwanza. 

Wawili hao walikaribisha binti yao Keilah Oyando duniani kupitia kurasa zao za mitandao ya kijamii.

Baada ya fanikio hilo, Mulamwah alichukua hatua ya kufungulia bintiye akaunti ya Facebook na ya  Instagram ( @keilah_oyando) ambazo tayari zimepata wafuasi 19,000 na 7,500 mtawalia siku moja tu baadae.

Hata hivyo, mchekeshaji huyo ambaye pia ni muuguzi si msanii wa kwanza kufungulia mtoto wake kurasa za mitandao ya kijamii.

Kunao baadhi ya wasanii wengine mashuhuri nchini ambao wanaendeleza kurasa za watoto wao za kijamii. 

1. Bahati na Diana Marua - Heaven Bahati, Majesty Bahati, Morgan Bahati

Mwanamuziki mashuhuri Kelvin Kioko almaarufu kama Bahati kwa ushirikiano na mpenzi wake Diana Marua wanaendeleza kurasa za mitandao ya kijamii za watoto wao watatu.

Akaunti ya @heavenbahati ina wafuasi zaidi ya laki tano, akaunti ya @majestybahati kwa sasa iko na wafuasi zaidi ya 250,000 huku @morgan_bahati ikiwa na wafuaki zaidi ya 162,000.

2. DJ Moh na Size 8 - Ladasha Belle Wambui, Muraya Jnr

Mcheza Santuri Samuel Muraya na mke wake mwanamuziki Linet Munyali almaarufu kama Size 8 walifungulia watoto wao wawili kurasa za mitandao ya kijamii.

Akaunti ya kifungua mimba wao  @ladashabellee.wambo kwa sasa ina wafuasi zaidi ya 422, 000 huku ya  @muraya.jnr ikiwa na wafuasi zaidi ya 62,000.

3. Tanasha Donna - Naseeb Junior

Naseeb Junior (2) ambaye ni mtoto wa mwanamuziki Tanasha Donna na staa wa Bongo Diamond Platnumz ni miongoni mwa watoto wa wasanii mashuhuri ambao wako na kurasa za mitandao ya kijamii.

Akaunti ya @naseeb.junior ya Instagram tayari iko na wafuasi zaidi ya laki mbili na picha 18 ambazo zimepakiwa.

4. Kabi Wajesus na Milly Wajesus

Wapenzi hao wawili ambao ni miongoni mwa Wakenya mashuhuri zaidi mitandaoni wana mtoto mmoja pamoja  ambaye anaitwa Reign Taji Kabi.

Kabi na Milly wanaendeleza akaunti ya @tajiwajesus kwenye mtandao wa Instagrma  ambayo kufikia sasa iko na wafuasi 178, 000.

5. King Kaka na Nana Owiti - Gweth Geezy

Mwanamuziki mashuhuri King Kaka pamoja na mpenzi wake Nana Owiti wanaendeleza akaunti ya binti yao kwenye mtandao wa Instagram.

Akaunti ya @gwethgeeezy ambaye ana miaka sita kwa sasa iko na wafuasi zaidi ya 27,000.