Binti ya Mulamwah ateuliwa kuwa balozi wa kampuni itakayogharamia mavazi yake hadi atimize miaka 17

Muhtasari

•Msanii huyo ambaye pia ni muuguzi amewashukuru mashabiki wote ambao wamemtumia jumbe za pongezi na zawadi kufuatia kuzaliwa kwa mtoto wao wa kwanza.

Image: INSTAGRAM// CAROL SONNIE

Masaa machache tu baada ya kuzaliwa, baraka zimeanza kumwandama mtoto wa mchekeshaji David Oyando almaarufu kama Mulamwah.

Keilah Oyando ambaye alizaliwa siku ya Jumapili ameteuliwa kuwa balozi rasmi ya kampuni kubwa ya kuuza nguo ya Kids Town.

Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Mulamwah alitangaza kuwa kampuni hiyo itagharamia mavazi ya bintiye hadi atakapotimiza miaka 17.

"Kujuana tu kidogo na malkia @keilah_oyando. Kwa sasa yeye ni balozi rasmi wa @kidstown_ke ambayo itamgharamia mavazi hadi afikishe miaka 17" Mulamwah aliandika.

Msanii huyo pia alichukua nafasi ile kuwashukuru mashabiki wote ambao wamemtumia jumbe za pongezi na kuwapa zawadi kufuatia kuzaliwa kwa mtoto wao wa kwanza.

"Asanteni sana kwa jumbe zenu za pongezi na zawadi. Tunashukuru kama familia na tunaomba Mungu awabariki sana" Alisema Mulamwah.

Siku ya Jumatatu mchekeshaji huyo pamoja na mpenzi wake Carolin e Muthoni walitangaza kuzaliwa kwa mtoto wao wa kwanza.

Wawili hao walitangaza mafanikio hayo kupitia kurasa zao za mitandao ya kijamii.

Kufuatia hatua hiyo, Mulamwah alimtunuku mpenzi wake shilingi laki moja kama zawadi ya kujifungua na kumwambia azitumie kukimu mahitaji yake binafsi.