"Mimi ni bidhaa zilizoharibika" Akothee azungumzia madhara ambayo umaarufu umemletea

Muhtasari

•Mama huyo wa watoto watano amesema kwamba anaogopa sana kukutana na watu hadharani na anatumai sana angekuwa mtu wa kawaida tu sio msanii mashuhuri.

•Akothee amesema kwamba mara nyingi amejipata akitorokea mashabiki wanaomkujia na nia ya kumsalimia kwa kuwa hapo awali amekutana na wengi ambao walijifanya kuwa nia njema ila wakageuka kuwa maadui wakubwa.

•Msanii huyo amewaomba mashabiki wake msamaha matendo yake na kudai kuwa hata yeye hayapendi na anatia juhudi kurekebisha

Image: INSTAGRAM// AKOTHEE

Mwanamuziki na mfanyibiashara mashuhuri Esther Akoth amefunguka kuhusu wakati mgumu ambao anapitia akiwa hadharani kutokana na umaarufu wake,

Mama huyo wa watoto watano amesema kwamba anaogopa sana kukutana na watu hadharani na anatumai sana angekuwa mtu wa kawaida tu sio msanii mashuhuri.

Akothee amesema kuwa ingawa huwa anaonekana kuwa mwanamke jasiri, amewahi kushuhudia mengi ambayo yamevunja moyo wake.

"Mimi ni bidhaa zilizoharibika. Nimegundua kwamba nimekuwa mtu anayewezwa na hisia sana hata sitaki tena kutoka nje ya nyumba yangu. Sipendi watu wakinitambua hadharani na kwa wakati mwingine huwa natamani tu ningekuwa mtu wa kawaida anayepita mitaani kwa amani" Akothee aliandika kwenye ukurasa wake wa Instagram.

Mwanzilishi huyo wa Akothee Safaris amesema kwamba mara nyingi amejipata akitorokea mashabiki wanaomkujia na nia ya kumsalimia kwa kuwa hapo awali amekutana na wengi ambao walijifanya kuwa nia njema ila wakageuka kuwa maadui wakubwa.

"Huwa naogopa sana nikipatana na mashabiki hadharani. Pindi ninapotambuliwa, hata bila kujua huwa nasimamisha shughuli na kutaka tu kutoroka. Si jambo la kuchekesha kwa kuwa najua labda wengine huwa na nia njema ila hata walionikujia hapo awali nilidhani wako na nia njema pia" Akothee alisema.

Mwanamuziki huyo amesema kwamba ako na mashabiki wengi wanaompenda na vile vile kuna wengi ambao hawampendi

Amekiri kuwa huwa anapatwa na wasiwasi mkubwa pindi anapotoka nyumbani kwake na kushuka kutoka kwa gari kwani hajui ambacho huenda kikatokea hadharani.

"Huwa nahisi kana kwamba tayari nimeshambuliwa hata kama hakuna mtu yeyote.Hisia hiyo imenigeuza kuwa mnyama na siku moja niliuliza mshauri wangu Bi Nyongo kama maisha yangu itawahi kuwa ya kawaida tena" Alisema Akothee.

Msanii huyo amewaomba mashabiki wake msamaha matendo yake na kudai kuwa hata yeye hayapendi na anatia juhudi kurekebisha.