Mwanahabari aomba usaidizi kukomesha jamaa anayetumia picha zake kupamba ukuta wa chumba chake

Muhtasari

•Mwanahabari huyo amedai kwamba hamfahamu jamaa huyo na hana uhusiano wowote naye

•Amesema kwamba amekuwa akimuonya jamaa huyo kwa muda  sasa ila inaonekana kana kwamba ametia masikio yake pamba.

Image: TWITTER// PURITY MUSEO

Msomaji wa habari katika runinga ya KBC Purity Museo ametoa ombi kwa Wakenya akitaka kusaidiwa kukomesha jamaa ambaye amepamba chumba chake na picha zake.

Kupitia ukurasa wake wa Twitter, Museo amedai kwamba jamaa anayejiita @FreeGerman2 amekuwa akimuwinda mitandaoni licha ya juhudi nyingi za kumzuia.

Museo amesema kwamba amechoshwa na jamaa huyo kwani kila anapomzuia kutoka kwa ukurasa wake huwa anaunda akaunti zingine na kuzitumia kupakia picha zake zaidi.

"Wakenya wenzangu. Nahitaji usaidizi wa kukomesha jamaa huyu! Ako na picha zangu kwenye chumba chake na kila ninapomzuia anaunda akaunti zingine na kuni'tag' kwenye chapisho zake" Museo alisema.

Mwanahabari huyo amedai kwamba hamfahamu jamaa huyo na hana uhusiano wowote naye. Amesema kwamba amekuwa akimuonya jamaa huyo kwa muda  sasa ila inaonekana kana kwamba ametia masikio yake pamba.

"Simjui mimi. Nimemuonya mara kadhaa ila haskii. Sioni likiwa jambo la kawaida" Alisema Museo.

Jamaa huyo anaonekana kuwa na mapenzi makubwa kwa mwanahabari huyo kwani amejaza picha zake kwenye akaunti yake.