Wa Jesus waeleza walivyokabiliana na chuki mitandaoni baada ya Kabi kufunguka kuhusu bintiye

Muhtasari

•Takriban miezi minne iliyopita Kabi alikiri kuwa na binti aliyepata pamoja na mwanadada aliyesemekana kuwa binamu yake.

•Wapenzi hao ambao walifunga ndoa mwaka wa 2017 walisema kwamba maombi na ushauri kutoka kwa  watu mbalimbali ziliwasaidia kukabiliana na chuki ambayo walipokea mitandaoni.

Image: INSTAGRAM// MILLY WA JESUS

Wanavlogu mashuhuri Peter Kabi na Milly Wambui wamefunguka kuhusu walivyokabiliana na kushambuliwa mitandaoni baada ya siri iliyokuwa imefichwa kwa miaka kujulikana hadharani.

Takriban miezi minne iliyopita Kabi alikiri kuwa na binti aliyepata pamoja na mwanadada aliyesemekana kuwa binamu yake.

"Ningependa kuthibitisha kwamba matokeo ya DNA yalitolewa jana  na kubaini kuwa mimi ndiye baba mzazi wa mtoto huyo. Matokeo yanasema kwamba mwaka wa 2013, kabla niokoke na nifunge ndoa nilimpata Abby" Kabi aliandika kwenye ukurasa wake wa Instagram mwezi Mei.

Wanamitandao wengi hawakupokea habari hizo vyema na wakamshambulia  sana msanii huyo anayejitambulisha kama Kabi wa Jesus.

Wakiwa kwenye mahojiano na Mungai Eve,wapenzi hao ambao walifunga ndoa mwaka wa 2017 walisema kwamba maombi na ushauri kutoka kwa  watu mbalimbali ziliwasaidia kukabiliana na chuki ambayo walipokea mitandaoni.

"Niliomba sana na nikaongea na watu. Tungezungumza na marafiki zetu, kuenda kushauriwa kwa sababu kuna mambo ambayo huja kama mtu hajatarajia" Milly alisema.

"Niliichukua kama changamoto ambayo kila mtu hupitia. Nilichokuwa naangazia ni moyo wake Kabi. Namjua kwani nimekaa naye kwa kipindi cha miaka minne ambayo imepita na namfahamu yeye ni nani. Namjua hajawahi badilika tangu tupatane. Hata kama mambo mengine yalifanyika hapo awali, kwangu niliamua kusimama naye kwani najua anafahamu moyo wake. Mimi hakuwa amenikosea kwa namna yoyote" Aliendelea kusema Milly.

Kabi alimshukuru sana mkewe kwa kusimama naye licha ya yote na kwa kumsaidia kukumbana na yaliyokuwa yamewapata.

"Niliomba sana. Hiyo stori sio rahisi. Ilitubidi tuombe sana na tutafute ushauri. Nashukuru Mungu kwa sababu ya mke wangu.  Alisimama nami na anaendelea kunisaidia hadi sasa. Nashukuru Mungu kwa sababu ya familia, marafiki na mke wangu. Hiyo ilikuwa maisha yangu ya kitambo na yeye hakuwa hapo. Lakini alikuwa tayari kukubali na kujadiliana nami ili kutatua yale" Kabi alisema