Njambi Koikai aghadhabishwa na uvumi kuwa alijaribu kujitoa uhai

Muhtasari

•Njambi ameghadhabishwa na madai ya uongo ambayo yalikuwa yamechapishwa mitandaoni kwamba amelazwa hospitalini baada ya kujaribu kujitoa uhai.

•Njambi alilaani mwandishi wa habari hizo za kivumi na kuomba aibu imupate kwa kuwa na mawazo mabaya juu ya maisha yake.

Image: INSTAGRAM// NJAMBI KOIKAI

MC mashuhuri wa reggea Njambi Koikai almaarufu kama Fyah Mama Njambi amepuuzilia mbali uvumi kwamba alikuwa amejaribu kujitoa uhai kitanzi.

Njambi ameghadhabishwa na madai ya uongo ambayo yalikuwa yamechapishwa mitandaoni kwamba amelazwa hospitalini baada ya kujaribu kujitoa uhai.

Msanii huyo amelaani kitendo hicho vikali kupitia ukurasa wake wa Instagram na kuagiza wale ambao wanaeneza uvumi kusita.

"Nimekuwa tu na jioni njema mahali na mamangu alafu mtu anaandika habari za kutisha. Tafadhali tahadhari na utumie mawazo kwa chochote unachofanya. Huu ni ujinga na haifai kusema kweli" Njambi amesema.

Msanii huyo ambaye alinusurika kutokana na maradhi ya Thoracic Endometriosis  amesema kwamba kwa sasa anajaribu kujenga maisha yake upya na kuomba apewe nafasi.

"Tafadhali nipeeni nafasi. Naishi maisha yangu, nafanya kazi, kujishughulisha na yanayonihusu na kujenga maisha yangu upya na nashukuru Mungu kwa kunipa nafasi nyingine ya kuishi. Hii inasikitisha lakini tazama yale ambayo Mungu atanitendea" Njambi alisema

Njambi alilaani mwandishi wa habari hizo za kivumi na kuomba aibu imupate kwa kuwa na mawazo mabaya juu ya maisha yake.