Facebook yaomba radhi kufuatia kukatizika kwa huduma za FB, WhatsApp na Instagram kwa masaa sita

Muhtasari

•Huduma hizo zilikatika usiku wa Jumatatu na mabilioni ya watumizi ambao waliathirika walibaki kushangaa tu kuhusu kilichokuwa kinaendelea.

•Kampuni hiyo imewashukuru watumizi wa huduma zake kwa kuwa na subira huku wakiahidi kuwa wanatia bidii kubwa kuhakikisha kuwa huduma zote zimerejea kikamili.

Image: RADIO JAMBO

Hatimaye huduma za Facebook, Instagram na WhatsApp zimeanza kurejea baada ya kukatizika kwa takriban masaa sita.

Huduma hizo zilikatika usiku wa Jumatatu na mabilioni ya watumizi ambao waliathirika walibaki kushangaa tu kuhusu kilichokuwa kinaendelea.

Hata hivyo kampuni ya Facebook ambayo inamilikiwa na bwenyenye Mark Zuckerberg imekiri kwamba wanafahamu kuwa kuna mabilioni ya watu ambao walizikosa sana huduma zao ambazo wanategemea kila siku.

Kupitia ujumbe uliochapishwa kwenye ukurasa rasmi wa Facebook, kampuni hiyo imeomba radhi kutoka kwa wote ambao waliathirika.

"Tungependa kukiri kwamba wengi ambao wanategemea huduma zetu kila siku wamethirika. Kwa biashara ndogo, makundi ambayo yanaleta watu pamoja , wabunifu ambao wanashirikisha jamii na familia zinazojaribu kuwa pamoja, samahani" Kampuni ya Facebook imeandika.

Kampuni hiyo imewashukuru watumizi wa huduma zake kwa kuwa na subira huku wakiahidi kuwa wanatia bidii kubwa kuhakikisha kuwa huduma zote zimerejea kikamili.

"Tunafanya kazi kwa bidii kurejesha huduma zetu na tuko na raha kuripoti kuwa 'apps' na huduma zetu zimeanza kurejea sasa. Asanteni kwa kutuelewa na kundelea kuwa pamoja na Facebook" Ujumbe huo ulisoma.

Mark Zuckerberg pia aliomba wanamitadao radhi kufuatia kuvurugika kwa huduma ambazo kampuni ambayo anamiliki hutoa huku akiahidi kurejea kwa huduma hizo.

"Facebook, Instagram, WhatsApp na Messenger zinarejea sasa. Poleni kwa kukatizika leo. Nafahamu jinsi mnavyotegemea huduma zetu ili kuwasiliana na watu ambao mnajali" Alisema Zuckerberg.

Kukatizika kwa huduma za Facebook, WhatsApp na Instagram kumeathiri sekta mbalimbali zikiwemo biashara, burudani, vyumba vya habari na isitoshe hali ya kutowasiliana huenda pia imethiri mahusiano kati ya watu ama makundi ya watu.