"Ndoa ni nzuri" Gavana Waiguru afunguka kuhusu ndoa yake, aeleza mbona huwa hawaonekani na mumewe hadharani

Muhtasari

•Waiguru alisema kuwa hatua ya kufunga pingu za maisha ambayo alipiga mwezi Julai mwaka wa 2019 ndiyo imefanya uso wake ukang'aa zaidi na akaongeza uzani wa mwili.

Image: MOSES MWANGI

Gavana wa Kirinyaga Anne Mumbi amesema kuwa anafurahia sana ndoa yake na wakili Kamotho Waiganjo.

Alipokuwa kwenye mahojiano katika stesheni ya NTV, mwanasiasa huyo alisema kuwa ndoa yake ya miaka mitatu inaendelea vyema na  imenoga.

Waiguru alisema kuwa hatua ya kufunga pingu za maisha ambayo alipiga mwezi Julai mwaka wa 2019 ndiyo imefanya uso wake ukang'aa zaidi na akaongeza uzani wa mwili.

"Ukiangalia sura utajua niko na furaha. Ukilinganisha kutoka ile siku nilifunga ndoa hadi sasa utaona nimeongeza kidogo. Inamaanisha kuwa niko na raha. Ndoa ni nzuri" Waiguru alisema.

Hata hivyo gavana huyo alilazimika kueleza kwa nini huwa haonekani na mumewe hadharani mara nyingi kama ilivyo kawaida ya wawili wapendanao.

Waiguru alisema kwamba mumewe amekuwa akisaidia katika uendeleshaji  shughulishi za kaunti huku akieleza kuwa kwa kawaida Bw. Waiganjo huwa hajihusishi sana na siasa.

"Huwa anafanya kazi yake kama mume wa gavana. Kama wikendi iliyopita, walikuwa na mpango wa afya. Walikuwa wanaanzisha mwezi wa saratani. Alikuwa mgeni mkuu na first ladies wengine walikuwa. Anafanya kazi yake vile anaweza  kusaidia kaunti lakini yeye sio mwanasiasa kwa hivyo sio kawaida umuone huko mbele" Waiguru alisema.