"Walisema tutakufia hospitalini na mtoto wangu" Vera Sidika asisitiza kuwa hatishwi kamwe na wenye chuki

Muhtasari

•Mpenzi huyo wa mwanamuziki Brown Mauzo amesisitiza kwamba angali amesimama kidete na hasumbuliwi na maneno ya watu.

•Amewashauri maadui wake kujitayarisha na chuki zaidi kwani anakadiria mengi mazuri ambayo yatawafanya wamuonee gere zaidi hivi karibuni.

Image: INSTAGRAM// VERA SIDIKA

Mwanasoshalaiti mashuhuri Vera Sidika ameapa kuwa hatishiwi kwa namna yoyote na wanaonena na kumtakia mabaya mitandaoni.

Kupitia ukurasa wake wa Instagram, mwanasoshaliti huyo amedai kuwa amekuwa akielekezewa chuki nyingi tangu alipopata ujauzito zaidi ya miezi minane iliyopita.

Hata hivyo mpenzi huyo wa mwanamuziki Brown Mauzo amesisitiza kwamba angali amesimama kidete na hasumbuliwi na maneno ya watu.

"Ninapofichua wenye chuki hapa haimaanishi kwamba jambo hilo linanisumbua. Huwa napokea jumbe nyingi za watu ambao wananiambia nisijisumbue. Hakuna chochote ambacho kinanisumbua... Huwa nawafichua ili muone jinsi watu walivyojawa na uchungu moyoni huko nje. Watu ata hawajali kama wewe ni mjamzito au la. Kama lolote lingekuwa linanisumbua basi ningekuwa nimelazwa hospitalini mara kadhaa juu ya kupandwa na presha.

Kutokwa mwezi wangu wa kwanza wa ujauzito kwa sababu ya drama zilizotokana na wenye chuki, baby mamas na watu wengine, miezi tisa sasa. Lakini bado niko salama kwa neema yake Mungu. Kama chuki haikunitikisa wakati huo basi hainiwezi sasa hivi" Vera alisema.

Mama huyo mtarajiwa amewasuta sana wenye chuki huku akidai kuwa huwa wanapendelea kuelekeza masikitiko yao kwa watu wengine.

Amesema kuwa yeye huwa hajalishwi na maneno yao kwani anaendelea vyema kabisa na maisha yake ya kifahari.

"Mnijaribu mwaka ujao. Wamesema hata mabaya zaidi. Hata walisema mtoto wangu atakufia hospitalini pamoja nami. Eti sitaweza kuponea. Lakini bado sijatishika kwani nyinyi wote sio Mungu. Ni Mungu ambaye anaamua, sio mabingwa wa kuandika" Alisema Vera.

Amewashauri maadui wake kujitayarisha na chuki zaidi kwani anakadiria mengi mazuri ambayo yatawafanya wamuonee gere zaidi hivi karibuni.

"Kama mnafikiria mmepata sababu tosha za kunichukia basi jitayarisheni. Kuna sababu nyingi ambazo zaja ili mnichukie zaidi. Mtaziona hivi karibuni kuanzia na reality show. Mtachukia lakini bado mnaendelea kutupatia kipato zaidi. Napenda" Vera alisema.

Mwanasoshalaiti huyo mwenye umri wa miaka 31 amedai kwamba wenye chuki wamemsaidia sana kupata  utajiri  zaidi kwani wamekuwa wakimfuata sana maishani wakitafuta sababu za kumchukia.