"Nimejeruhiwa na naumia" Mwanaharakati Boniface Mwangi azungumza baada ya kushambuliwa na GSU

Muhtasari

•Mwangi amesema kuwa anaendelea vyema ila anashuhudia maumivu kiasi kwani aliugua majeraha kutokana na kipigo alichopokea.

•Licha ya yaliyomkumba siku ya Ijumaa,  baba huyo wa watoto watatu ameapa kuwa hatasita kupaza sauti yake kila anaposhuhudia udhalimu ukiendelea.

Image: INSTAGRAM// BONIFACE MWANGI

Mwanaharakati Boniface Mwangi ametoa shukran kwa wote ambao wamefanya hatua ya kumjulia hali baada yake kudai kuwa alishambuliwa vibaya na maafisa wa GSU kwa kuwarekodi wakinyanyasa raia.

Mwangi alisema kuwa mzozo ulianza wakati jamaa waliojitambulisha kama maafisa wa KRA na maafisa wa GSU walianza kukamata wafanyibiashara kiholela. Alisema kuwa 'maafisa' hao walikosa kutoa vitambulisho vya kazi walipoagizwa na hapo ndipo mabishano yakaanza.

Kulingana na Mwangi, maafisa wa GSU ambao alirekodi wakitendea raia hujuma walimtaka awakabidhi simu ambayo alitumia kurekodi ila akasita na kutoroka.

Hata hivyo bahati haikuwa upande wake kwani baada ya kupiga hatua chache alianguka chini na maafisa ambao walikuwa wamejawa na ghadhabu wakamkamata na kumshambulia kwa viboko na mateke.

Mwangi alipakia video ambayo ilionyesha matukio hayo kwenye kurasa zake za mitandao ya kijamii.

Wanamitandao wengi walijumuika kumfariji mwanaharakati huyo kwa yaliyotukia huku wengine wakitaka kujua alivyokuwa anaendelea kiafya baada ya tukio hilo la kuhofisha.

Mwangi amesema kuwa anaendelea vyema ila anashuhudia maumivu kiasi kwani aliugua majeraha kutokana na kipigo alichopokea.

"Nawashukuru kwa maneno yenu mazuri, jumbe zenu na simu ambazo nimepokea. Naumia kiasi na niko na vidonda ila niko sawa" Mwangi amesema kupitia ukurasa wake wa Twitter.

Licha ya yaliyomkumba siku ya Ijumaa,  baba huyo wa watoto watatu ameapa kuwa hatasita kupaza sauti yake kila anaposhuhudia udhalimu ukiendelea.

Mwanaharakati huyo amewasihi Wakenya kutokubali kudhulumiwa na kuwataka wawe na ujasiri wa kulalamika kila wanapodhulumiwa.

"Sitawahi kubali kunyamaza wakati ninapoona udhalimu ukiendelea mahali popote. Endeleeni kuongea kwa ujasiri bila kusita!" Mwangi alisema.

Shirika la KRA pia limezungumza kufuatia tukio hilo huku wakisisitiza kuwa maafisa wake wanahitajika kubeba vitambulisho kila wanapoenda kufanya operesheni yoyote.

"Mjue kuwa maafisa wa KRA ambao  wako katika zamu lazima wabebe vitambulisho wanapoingia kwenye makao yoyote ya biashara. Umma unafaa kutumia mfumo wetu kuthibitisha maafisa wa KRA." KRA ilisema kupitia mtandao  wa Twitter.