'Asanteni kwa uvumilivu,'Otile Brown azungumza baada ya kibao chake na Jovial kurejeshwa Youtube

Muhtasari
  • Otile Brown azungumza baada ya kibao chake na Jovial kurejeshwa Youtube

Baada ya nyimbo zake tano kufutwa kutoka mtandao wa YouTube, mwanamuziki Jacob Obunga almaarufu kama Otile Brown alijitokeza kuwasuta vikali waliotekeleza kitendo hicho.

Hii leo(Jumanne) amewashukuru mashabiki wake kwa uvumilivu wao baada ya kuamkia siku ya Jumatano wiki jana na kupata vibao vyake kadhaa haviko kwenye youtube.

Siku ya Jumatano wanamitandao waliamkia habari kwamba nyimbo za Otile Brown k.v. Dusuma, Chaguo la Moyo, Such Kinda Love, Hi na Aiyana hazikuwepo YouTube tena.

Brown alisema kwamba anafahamu mhusika aliye nyuma ya kitendo hicho huku akitishia kulipiza kisasi punde atakapomaliza kukusanya ushahidi.

"Hata sijakasirika, nimesitikishwa na watu wangu. Hawa ni Wakenya ambao wanafanya haya. Ulidhani unafanya kazi, pia sisi tunafanya kazi. Tunakujua tayari lakini nakuahidi tutakapopata ushahidi utajua nguvu zetu pia. Hata wewe hutakula. Tatizo ni kwamba una roho mbaya, tukiamua kuwa na roho mbaya kama wewe hapa hapatakalika msee. Usione tumenyamaza ukachukulia poa msee" Otile Brown alisema.

Kibao chake na msanii Jovial cha 'such kind of love' kimerejeshwa kwenye youtube.

Kupitia kwenye ukurasa wake wa instagram aliwafahamisha mashabiki wake kuhusu kurejeshwa kwa kibao chake.

"Na tumerudi kwenye Youtube asanteni kwa uvumilivu 🙏🏼❤️ riziki wataichelewesha tu 😊 .. watch me #justinlovemusic #wegotnothingbutlove go watch your favs ❤️," Aliandika Otile.

Ni kibao ambacho kilikuwa kimepokea watazamaji zaidi ya milioni 10 kwa miezi 4.