"Hakuna aliye na mwongozo wa kuishi maisha bila dosari" Akothee awasuta wanaoeneza chuki dhidi ya watu mashuhuri

Muhtasari

• Mama huyo wa watoto watano amesema kuwa huwa anashangazwa sana na  maneno ya kikatili ambayo baadhi ya wanamitandao huelekezea watu mashuhuri.

•Hata hivyo ameeleza kuwa hakuna yeyote anayeweza kuishi maisha bila doa na kuwashauri celebs wengine wasitishwe na maneno ya watu.

Image: INSTAGRAM// AKOTHEE

Mwanamuziki na mfanyibiashara mashuhuri nchini Esther Akoth almaarufu kama Akothee amewasherehekea watu mashuhuri maarufu kama 'celebs' wenzake kwa yale yote ambayo wamelazimika kustahimili mbele ya jamii.

Hali kadhalika, msanii huyo mwenye umri wa mika 41 amewasuta sana wakosoaji ambao wana mazoea ya kueneza chuki dhidi ya watu mashuhuri.

Kupitia ukurasa wake wa Instagram, mama huyo wa watoto watano amesema kuwa huwa anashangazwa sana na  maneno ya kikatili ambayo baadhi ya wanamitandao huelekezea watu mashuhuri.

Amelalamikia maneno ya kikatili ambayo aghalabu huelekezewa watu mashuhuri huku akidai kuwa anashangaa ikiwa bado kuna watu wenye utu duniani.

"Niruhusu nibusu celebs wote kwenye usanii.. Mungu wangu, ninapoangalia maoni ya kikatili dhidi ya watu mashuhuri, huwa nashangaa iwapo bado kuna binadamu walio hai.. Kama hauna mtoto wanakutusi, ukiwa na ujauzito wanakutusi na wanakutakia mabaya, unapata ujauzito bila mwanaume yeyote maishani mwako wanakutusi, unapoteza mtoto wanakutusi, unapata mtoto kabla muda wake haujafika wanakutusi.. unapoteza kazi yako wanakutusi.. unaonyesha ndugu zako wanakutusi.. unachumbia mwanaume mzee, hawahissi mapenzi, wanakutusi, unachumbia mtu mdogo  tena hawana raha wanakutusi sanaa" Akothee alisema.

Akothee amesema kuwa amegundua kuwa wakooaji wengi hawana kazi na hawana matumaini maishani na ndiposa wanatumbuizwa na maisha ya wengine.

Hata hivyo ameeleza kuwa hakuna yeyote anayeweza kuishi maisha bila doa na kuwashauri celebs wengine wasitishwe na maneno ya watu.

"Nimekuja kugundua kuwa watu hawa hawamaanishi kile wanachosema, hawana kazi na wako na chuki. Maisha yao yamesimama na yako ndio burudani. Furahia maisha na uendelee.

Hakuna aliye na mwongozo wa kuishi maisha bila kasoro, hata wale wanaotusiana. Kwa kweli maisha yao yameharibika zaidi, ni vile tu hakuna watu wanaowajua. Endelea hivo hivo, unafanya vyema" Alisema Akothee.

Mwanamuziki huyo ni miongoni mwa watu mashuhuri ambao wamekosolewa sana mitandaoni kutokana na mtindo wa maisha yake.

Mahusiano ambayo amewahi kujitosa ndani yake ni kati ya mambo ambayo wakosoaji wengi wametumia kumkashifu na kumuelekezea maneno ya matusi.

Mwanasoshalaiti Vera Sidika pia hajasazwa, amekuwa akipokea chuki nyingi mitandaoni haswa baada ya hatua  ya kutangaza ujauzito wake mapema mwaka huu.