'Zingatia kazi yako, mahusiano yatakupa matokeo ya kusikitisha,' Diamond Platnumz atoa ushauri

Muhtasari

•Baba huyo wa watoto wanne wanaojulikana amesema kwamba kwa kawaida mtu anapozingatia mahusiano zaidi huishia katika hali ya masikitiko.

•Licha ya mafanikio yake makubwa kwenye sanaa ya muziki, Diamond hajaweza kufanikiwa katika mahusiano kufikia sasa.

Image: INSTAGRAM// DIAMOND PLATNUMZ

Staa wa Bongo Diamond Platnumz amewashauri vijana kuzingatia kazi zao zaidi ya mahusiano.

Kupitia ukurasa wake wa Instagram, mwanamuziki huyo amesema kwamba kazi pekee ndio yaweza kupatia mtu matokeo chanya.

Baba huyo wa watoto wanne wanaojulikana amesema kwamba kwa kawaida mtu anapozingatia mahusiano zaidi huishia katika hali ya masikitiko.

"Zingatieni kazi zenu kwa sababu matokeo yatakuwa mema. Lakini unapozingatia mahusiano matokeo yatakuwa mabaya na ya kusikitisha. Sikia kutoka kwa simba" Diamond alisema.

Msanii huyo mzaliwa wa Tanzania ni miongoni mwa wanamuziki bora zaidi barani Afrika na kote duniani kutokana na idadi kubwa ya mashabiki wanaopendezwa na ngoma zake. 

Mapema mwaka huu mwanamuziki huyo aliteuliwa kupokea tuzo la kimataifa la BET ingawa akapoteza kwa Burna Boy wa Nigeria.

Licha ya mafanikio yake makubwa kwenye sanaa ya muziki, Diamond hajaweza kufanikiwa katika mahusiano kufikia sasa.

Msanii huyo mwenye umri wa miaka 32 tayari amechumbia zaidi ya wanawake 10 kufikia sasa na kupata watoto na watatu wao ila hakuna ndoa yake iliyoweza kudumu.

Miongoni mwa wanawake ambao Diamond anaaminika kuchumbia ni pamoja na Hamisa Mobetto, Wema Sepetu, Zari Hassan,Jacque Wolper, Jokate Mwegelo, Irene Uwuoya,Tanasha Donna kati ya wengine.

Mwanamuziki huyo ana watoto wawili aliopata na mwanasoshalaiti mzaliwa wa Uganda Zari Hassan, mmoja na Hamisa Mobetto na mwingine mmoja na mwanamuziki kutoka Kenya Tanasha Donna.