Nyota wa sinema Alec Baldwin amuua mwanamke kutumia bunduki wakati wa kutengenezwa kwa filamu yake

Muhtasari

•Mwanamke alikufa na mwanaume kujeruhiwa baada ya muigizaji Alec Baldwin kufyatua risasi kutumia bunduki ya maigizo kwenye seti ya filamu huko New Mexico.

•Msemaji wa Bw Baldwin aliliambia shirika la habari la AP kwamba kisa hicho kilihusisha utumiaji mbaya wa bunduki ya maigizo.

Image: GETTY IMAGES

Mwanamke amekufa na mwanaume amejeruhiwa baada ya muigizaji Alec Baldwin kufyatua risasi kutumia bunduki ya maigizo kwenye seti ya filamu huko New Mexico.

Polisi katika jimbo hilo la Marekani walisema Bw. Baldwin alitoa silaha hiyo wakati wa utengenezaji wa filamu yake

Mwanamke huyo alipelekwa hospitalini lakini alifariki kutokana na majeraha yake. Mwanaume aliyejeruhiwa -mkurugenzi wa filamu, alikuwa akipokea huduma ya dharura.

Msemaji wa Bw Baldwin aliliambia shirika la habari la AP kwamba kisa hicho kilihusisha utumiaji mbaya wa bunduki ya maigizo.

Mwanamke huyo ametajwa kama Halyna Hutchins, 42, ambaye alikuwa akifanya kazi kama mkurugenzi wa upigaji picha. Mtu anayetibiwa ni Joel Souza, 48, mkurugenzi wa filamu.

Polisi bado wanachunguza tukio hilo huko Bonanza Creek Ranch, eneo maarufu la utengenezaji wa sinema, na hakuna mashtaka yoyote yaliyofunguliwa.