"Nitakupa maua yako ukiwa hai juu unastahili" Baby Mama wa Bahati, Yvette amsifa Diana Marua anapoadhimisha siku ya kuzaliwa

Muhtasari

•Mke huyo wa mwanamuziki mashuhuri Kelvin Kioko almaarufu kama Bahati anasherehekea kufikisha miaka 32.

•Yvette ambaye ana mtoto mmoja na Bahati amemlimbikizia Diana sifa kochokocho huku akimhakikishia kuwa anampenda sana na kumthamini.

Yvette Obura na Diana Marua
Yvette Obura na Diana Marua
Image: INSTAGRAM

Hivi leo Diana Marua anaadhimisha siku yake ya kuzaliwa.

Mke huyo wa mwanamuziki mashuhuri Kelvin Kioko almaarufu kama Bahati anasherehekea kufikisha miaka 32.

Mamia ya wanamitandao na mashabiki wake  wameendelea kumtumia Diana jumbe za kheri za kuzaliwa na kumtakia maisha marefu.

Aliyekuwa mpenzi  Bahati Yvette Obura hajasazwa nyuma katika kumtakia mama huyo wa watoto wawili kheri za kuzaliwa.

Yvette ambaye ana mtoto mmoja na Bahati amemlimbikizia Diana sifa kochokocho huku akimhakikishia kuwa anampenda sana na kumthamini.

"Siku njema ya kuzaliwa Mama Heaven @diana_marua. Siku ya leo nataka ujue kuwa nakuthamini, nakupenda na na nashukuru Mungu kwa sababu yako. Umekuwa mtu asiye na ubinafsi, mwenye kuelewa, mkarimu, mwenye upendo, mwenye kujali, sio tu kwa @mueni_bahati ila kwa watu wote waliokuzunguka" Yvette amesema kupitia ukurasa wake wa Instagram.

Yvette amemsherehekea Diana huku akimtakia mengi mema maishani.

"Naomba katika umri wako mpya kikombe chako kiendelee kujawa na amani, upendo, fadhila, na mafanikio. Tunakupenda sana na nitakupatia maua yako ukiwa hai kwa sababu unayahitaji. Siku ya kuzaliwa yenye furaha @diana_marua" Yvette amesema.